Friday, April 14, 2017

WAJASILIMALI WA KILIMO CHA BIASHARA VISIWANI PEMBA WASHAURI KUWA NA MAWASILIANO NA WAKULIMA WENZAO

DSC_1638
Na Masanja Mabula -Pemba ..
 
WAJASIRIAMALI wa kilimo cha biashara nchini, wameshauriwa kuwa na mawasiliano ya karibu miongoni mwao, ili kuepusha kulima na kuvuna kilimo cha aina moja na kukosa soko la uhakika la bidhaa zao.
 
Ushauri huo umetolewa, na Mkurugenzi wa Ushirika kutoka Wizara ya Kazi, Uwezeshaji, Wazee, Vijana, Wanawake na Watoto Khamis Daud Simba, alipokuwa akizungumza kwenye mafunzo ya kuzijengea uwezo redio jamii kisiwani Pemba, ili kuandaa vipindi vya kuwaelimisha wananchi juu ya ujio wa Saccos za wilaya.
 
Alisema, wajasiriamali wamekuwa mstari wa mbele kulima kilimo cha mboga mboga kwa ajili ya biashara, ingawa wamekuwa wakikosa soko la uhakika, kutokana na kulima na kuvuna kwa pamoja.
 
Mkurugenzi huyo alieleza kuwa, kama wakiwa na mawasiliano ya pamoja, watajipangia kwa kupishana, jinsi ya ukulima kwa kutangulia kundi moja na kisha jengine kufuata.
 
“Kama wajasiriamali wa kilimo wakiwasiliana juu ya kilimo, na kuacha mtindo wa kulima na kuvuna kwa pamoja, basi soko linaweza kuwa hafifu kwa wateja kuzidiwa na bidhaa’’,alifafanua.
 
Katika hatua nyengine Mkurugenzi huyo, amewataka wananchi waliojiunga kwenye Saccos ndogo ndogo, kujipanga vyema, ili kuzitumia vyema Saccos za kila wilaya zao.
 
Akifungua mafunzo hayo, Naibu waziri wa Kazi, Uwezeshaji, Vijana, Wazee, Wanawake na Watoto Shadya Mohamed Suleiman, amewataka waandishi wa habari kuwaelimisha wananchi, juu ya ujio wa Saccos za wilaya.
 
“Nyinyi waandishi wa habari, tunawategemea sana katika kuwafikia wananchi na kuwaelimisha kuwa, sasa serikali inataka kutanua wigo wa kuwainua kiuchumi, kwa kuwepo kwa Saccos ya wilaya’’,alifafanua.
 
Nae Naibu Katibu Mkuu, anaeshughulia wanawake na watoto Zanzibar Mauwa Makame Rajab, alisema redio za jamii zinamchango mkubwa, katika kufikia malengo ya wanajamii husika.
 
“Wizara kwa makusudi, imeamua kuwapa mafunzo ya siku moja ya utayarishaji wa vipindi vyenye kuelimisha jamii, juu ya ujio wa Saccos za wilaya”,alifafanua.
 
Meneja redio jamii Mkoani Ali Abass Omar, ameahidi kuwa watawaelimisha wananchi, juu ya azma ya serikali katika kuanzisha Saccos za wilaya.
 
Hata hivyo mtangaazaji wa ZBC redio Khadija Kombo Khamis, amepongeza hatua ya Idara ya vyama vya ushirika kuwashirikisha kikamilifu, ili kuwaelimisha wananchi.
 
Idara ya vyama vya ushirika Zanzibar, inakusudia kuanzisha kwa Saccos za kila wilaya Unguja Pemba, ili wananchi wawe na mitaji mikubwa, huku wakizitumia redio jamii za Mkoani na Micheweni kuwaelimisha wananchi

No comments:

Post a Comment

Fahamu mbinu za kuongeza thamani nyama

  Safari ya kuongeza thamani nyama ya mifugo huanzia shambani kwa usimamizi wa ufugaji na uzalishaji. Lishe bora ni muhimu kwa wa ufugaji ...