RC DKT. KEBWE STEPHEN KEBWE AMUAGIZA MKUU WA WILAYA YA KILOMBERO JAMES IHUNYO KUKAA NA VIONGOZI WA HALMASHAURI ZA KILOMBERO KUTAFUTA NJIA YA KUKITUMIA KITUO CHA UTAFITI NA MAFUNZO YA KILIMO

Image result for shamba la mpunga
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro  Dkt. Kebwe Stephen Kebwe amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kilombero James Ihunyo kukaa na viongozi wa Halmashauri za Kilombero na Mji wa Ifakara ili kutafuta njia ya kukitumia vema Kituo cha Utafiti na Mafunzo ya Kilimo KATRIN kilichopo Wilayani humo ili kuleta mapinduzi ya Kilimo kwa Halmashauri zake.
Dkt. Kebwe ametoa agizo hilo Februari 21 mwaka huu, wakati wa ziara yake Wilayani Kilombero baada ya kutembelea Kituo cha Utafiti na Mafunzo ya Kilimo KATRIN na kuongea na Uongozi wa kituo hicho.
Amesema, uwepo wa Kituo cha Utafiti na Mafunzo ya Kilimo Wilayani humo ni fursa kubwa katika masuala ya kilimo na hivyo Halmashauri zilizopo katika Wilaya hiyo zinatakiwa kufanya kila jitihada na kutafuta njia za kufaidi matunda ya chuo hicho hasa katika kilimo na hivyo kuonesha utofauti na maeneo mengine ambayo hayana vituo vinavyojishughulisha na kilimo.
Kwa sababu hiyo, amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Kilombero James Ihunyo kuitisha Kongamano la wadau wa kilimo ngazi ya Wilaya na kuona ni kwa namna gani kituo hicho kinaweza kuboresha kilimo katika Halmashauri zake mbili za Kilombero na Halmashauri ya Mji wa Ifakara.
 “DC mimi nakupa maagizo leo, fuatilia huyo Mkurugezi ili kuona ni kwa vipi anatumia vyuo tulivyo navyo hapa katika kuleta mapinduzi ya kilimo” Dkt. Kebwe alisema.
Aliongeza kuwa, Kongamano la wadau wa Kilimo ngazi ya Mkoa limeshafanyika  wiki moja iliyopita na kwamba katika kongamano hilo aliagiza kila Wilaya ifanye Kongamano la wadau wa Kilimo ngazi ya Wilaya, kwa lengo la kujadili namna ya kuinua uzalishaji katika Sekta ya Kilimo. Hivyo amemtaka Mkuu huyo wa Wilaya atumie fursa hiyo kujadili pia suala la chuo hicho kitakavyoleta mapinduzi ya kilimo Wilayani humo.
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa alimuagiza Kaimu Mkuu wa Kituo hicho Bw. Jerome Mgase, kuwa anataka chuo hicho kujipanga katika kusaidia Halmashauri za Kilombero na Mji wa Ifakara na kujielekeza katika eneo la kuinua uzalishaji katika sekta ya Kilimo.
Ameshauri kuwa wanafunzi wa mwaka wa pili wanapokaribia kuhitimu na kufanya mazoezi yao wapangiwe Vijiji au Vitongoji mbalimbali katika Halmashauri hizo ili kulea mashamba darasa yaliyopo na kuwafundisha wananchi kilimo bora kwa Vitendo.
Dkt. Kebwe amesema, wananchi kwa sasa wanataka kufundishwa kilimo bora kwa vitendo ili kuona utofauti wa kilimo cha mazoea walichokuwa wanakitumia siku zote na kilimo bora kwa kuona uzalishaji wake unaongezeka wakilinganisha na hapo awali.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilombero James Ihunyo amesema, anayapokea maagizo ya Mhe. Mkuu wa Mkoa, hata hivyo aefafanua kuwa  alishawaagiza wakurugenzi wa Halmashauri zote mbili kuangalia maeneo ambayo chuo hicho kingeweza kuwasaidia  katika kupata mbegu bora za Mpunga au  kuongeza zaidi uzalishaji wa mazao.
Pamoja na kutekeleza agizo hilo anasema pia atajikita katika kutatua mgogoro wa muda mrefu uliopo baina ya chuo hicho na Wananchi zaidi ya 200 ambao inasemekana wengine wamevamia maeneo ya chuo katika maana ya makazi na wengine  kwenye mashamba ya chuo ili kukaa katika meza moja na kupata suluhisho la kudumu.
Kituo cha Utafiti na Mafunzo ya Kilimo KATRIN (Kilombero Agricultural Training and Reseach Institute) ambacho kipo chini ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na maendeleo ya Uvuvi, kipo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero Wilayani Kilombero, kilianzishwa mwaka 1963 kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanganyika (kwa wakati huo) na Ujerumani.
Kituo kilikuwa na jukumu la kufanya tafiti za mazao mbalimbali yakiwemo ya mahindi, mtama, ulezi, ufuta, alizeti, minazi na pamba. Mazao mengine ni  mikunde, mazao ya mafuta, mbogamboga na matunda. Mwanzoni mwa miaka ya themanini kituo kilipewa jukumu la kuratibu utafiti wa mpunga Kitaifa.
Kwa matokeo mazuri yaliyotokana na kituo hicho, mnamo mwaka 2010, KATRIN ilichaguliwa kuwa kituo mahiri cha mpunga kwa nchi za ukanda wa Mashariki mwa Afrika (Regional Rice Centre of Excellence – RRCoE) na hadi sasa Kituo kimefanikiwa kufanya utafiti na kupitishwa kwa mbegu kumi kitaifa.

Comments

Popular Posts