Nafasi ya kupanda mpunga

 Kama unatumia mbegu za asili, panda mpunga kwa kutumia nafasi ya sm 20 kwa sm 20 au sm 25 kwa sm 25 au sm 30 kwa sm 30.

Na ikiwa unatumia mbegu bora inashauriwa kutumia nafasi ya sm 15 kwa sm 15 au sm 20 kwa sm 20.

Kwenye mpangilio wa mistari miwili miwili (double rows), nafasi kati ya mistari miwili ni sm 10, na nafasi kati ya mimea katika kila mstari ni sm 20, na nafasi kati ya mistari miwili na mistari miwili mingine (double rows) ni sm 40.

Kupanda kwa nafasi ni kati ya njia bora za kilimo inayomwezesha mkulima kupata mazao bora. Hivyo ni muhimu sana kuzingatia kupanda kwa mistari na kufuata nafasi zinazoshauriwa na wataalamu wa kilimo.


Muda wa kupanda unatofautiana kutoka eneo moja hadi jingine kulingana na majira ya mvua.

Kwa mfano katika wilaya ya Morogoro tarehe za kupanda ni kuanzia Desemba hadi Januari kwa mpunga wa muda mrefu.

Kwa mpunga wa muda wa kati na muda mfupi, tarehe za kupanda ni Februari hadi Machi.

Kupalilia Mpunga

Ni muhimu shamba lipaliliwe ili kuondoa magugu. Magugu ni mimea hivyo hushindana na mimea iliyopandwa na mkulima kwa kunyonya virutubisho ardhini. Magugu yanaweza pia kuhifadhi wadudu na magonjwa yanayoweza kushambulia mimea iliyopandwa na hivyo kupunguza mavuno.

Katika kilimo cha mpunga, ni muhimu shamba lipaliliwe siku 14 hadi 21 baada ya mimea kuota kufuatana na hali ya shamba wakati wa kupanda. Ni vizuri katika kilimo cha mpunga, shamba lipaliliwe mara mbili, kutegemeana na hali ya magugu katika shamba. Unaweza kupalilia kwa kung’olea kwa mkono, kwa mashine au kwa kutumua viua magugu (herbicides) kama vile 2, 4-D (Two Four D).

Utafiti unaonyesha kwamba, shamba la mpunga ambalo halijapaliliwa linaweza kupunguza mavuno kwa asilimia 60 hadi 100 ya mavuno yanayotarajiwa. Hata kama mkulima atatumia mbegu bora, aina na kiasi cha mbolea zinazoshauriwa, kupanda kwa mstari pamoja na mbinu nyingine bora zinazoshauriwa, bila kupalilia hali hii itaathiri mavuno yake.


Mbolea za kukuzia mpunga

Ni mbolea zinazotumika baada ya mimea kuota kwa lengo la kuikuza mimea ili itoe mavuno bora. Mara nyingi mbolea hizi zinatoa kirutubisho cha naitrojeni. Kiwango kinachopendekezwa ni kilo 60 naitrogeni kwa hektari, ambacho ni sawasawa na kiasi cha mifuko miwili ya UREA au Minne na Nusu Ya CAN au Mitatu ya SA. Mbolea inayotumika mara kwa mara ni Urea. Hata hivyo mbolea zingine kama SA inaweza kutumika kama kuna mahitaji ya salfa. CAN inaweza kutumika kama kuna mahitaji maalum ya nitrate na ammonium. Kwenye mpunga, mbolea ya kukuzia inawekwa wiki mbili baada ya kupandikiza miche na irudie tena baada ya wiki nne.

Kuweka mbolea: Mbolea ya kukuzia hutiwa kwa kusia wiki mbili baada ya kupandikiza, na kurudia mwezi mmoja baadaye. Ni vyema kuweka mbolea za kukuzia mara mbili ya kiasi kinachopendekezwa.

Shamba-la-Mpunga-uliopandikizwa
Shamba la mpunga uliopandwa kwa mistari

Kudhibiti Magonjwa na Wadudu Wanaoshambulia Mpunga

Magonjwa Yanayoshambulia Mpunga

Magonjwa ya mpunga yamegawanyika katika makundi matatu kulingana na vimelea visababishi ambavyo ni fungasi, virusi na bakteria.

i) Rice blast (Ukungu)

Unaosababishwa na Pyricularia oryzae.

Dawa/Kudhibiti: Mbegu bora inayostahimili ugonjwa, kupanda mapema, kung’oa mimea iliyoathirika ama kunyunyiza dawa za kuua ‘vectors’ kama vile inzi weupe (white flies).

ii) Brown leaf spot

Unaosababishwa na Helminthosporium spp.

Dawa/Kudhibiti: Panda mbegu kwa udongo unaofaa, weka mbolea ya kuzuia au tibu mbegu na dawa.

iii) Sheath rot

Unaosababishwa na Acrocylindrium oryzae.

Dawa/Kudhibiti: Kwa sasa hakuna njia ya kuzuia

iv) Rice Yellow Mottle Virus (RYMV) – Kimnyanga

Hivi karibuni ugonjwa wa kimyanga umetajwa kama ugonjwa hatari sana kwa mpunga hapa Tanzania.

Dawa/Kudhibiti: Panda mbegu zilizoboreshwa, zinazostahimili magonjwa au ng’oa mimea iliyoathirika.

Magonjwa yasababishwayo na bakteria nayo wametajwa kuwa na madhara makubwa kwa uzalishaji wa mpunga hapa nchini. Bakteria hawa wanajumuisha Acidovorax avenae subsp. Avenae asababishae ugonjwa wa bacterial stripe, Pantoea aglomerans, asababishae ugonjwa wa palea browning na Xanthomonas oryzae p.v. oryzae.

Wadudu wanaoshambulia mpunga

Kuna aina nyingi sana za wadudu wanaoathiri mpunga katika hatua mbalimbali za ukuaji wa mpunga. Wanapokithiri na wasipodhibitiwa hupunguza kiasi cha mavuno shambani.

i) White flies (Funza weupe)

Dawa/Kudhibiti: Nyunyiza dawa ya Thiodan, Endosulfan (Thionex), Fipronil (k.m. Regent 3G), Fenthion (k.m. Lebaycid)

ii) Rice stalk borer waharibifu

Kudhibiti: Nyunyiza dawa ya Thiodan, Endosulfan (Thionex), Fipronil (k.m. Re­gent 3G), Fenthion (k.m. Lebaycid) Ili mkulima aweze kupata mazao mengi na bora inashauriwa kutumia dawa za kuzuia magonjwa na wadudu wanaoshambulia mimea na njia zinginezo.


Kuvuna, Kukausha, Kusafisha na Kuhifadhi Mpunga

Kuvuna: Mpunga uko tayari kuvuna wakati asilimia themanini (80%) ya rangi ya mpunga kwenye masuke imebadilika na kuwa dhahabu. Mpunga unavunwa kwa kukata bua pamoja na suke lake.

Kuvuna-mpunga-kwa-siko

Uvunaji wa mpunga

Kukausha: Rundika pahali pakavu k.m. kwenye tuta la jaruba halafu pigapiga (thresh) ili kutenganisha masuke na mpunga. Kama mpunga hayajakauka vizuri hukaushwa zaidi juani kwa siku 3-4 ili kupunguza unyevunyevu kufikia kiwango kinachofaa kwa kuhifadhi (14%). Ni muhimu mpunga ukauke vizuri ili usioze ukiwekwa ghalani.

Kusafisha: Mpunga uliyokauka vizuri hupepetwa na vilevile mapepe huondolewa. 

Kuhifadhi: Mpunga safi huwekwa kwenye gunia na magunia kupangwa vizuri ghalani juu ya mbao yasiguse sakafu.


Comments

Popular Posts