Wafahamu Panya Waharibifu Wa Mazao Shambani

 Panya ni wanyama wadogo jamii ya mammalia walio katika familia/kundi linalotambulika kitaalamu kama Muridae wenye meno mawili ya mbele kwa kila taya na mwanya kati ya meno ya mbele na magego unaotambulika kitaalamu kama Diastema.

Panya mbali na wadudu waharibifu wa mazao pamoja na magugu huhesabika kama mojawapo ya visumbufu vya mazao kutokana na madhara na hasara wanazoweza kumsababishia mkulima.

Aina Za Panya

Duniani kote kuna aina takribani 2500 za panya wenye rangi, ukubwa na maumbile tofauti kulingana na aina zao ambapo idadi yake inaendelea kuongezeka siku baada ya siku. Kwa upande wa Tanzania kuna aina za panya si chini ya aina ishirini ambapo baadhi yao ni kama vile panya shamba, panya michanga, panya miraba, panya wa darini, panya mbilikimo, kiruka njia, sengi na panya miiba. Katika makala hii sitoweza kuzielezea aina zote bali nitaangazia aina za panya zinazoweza kusababisha hasara kubwa na zinazopatikana karibu mikoa yote nchini. Aina hizi za panya ni kama zifuatazo;

 

  1. Panya Shamba (Mastomys natalensis)

Panya shamba ni aina ya panya waharibifu wanaosababisha hasara kubwa kwa wakulima hasa walio katika nchi zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara na hupendelea kuishi porini na mashambani wakiwa na uwezo wa kuzaa na kuongezeka kwa wingi kwa kipindi cha muda mfupi. Katika mazingira yanayowafaa majike wa aina hii ya panya wana uwezo wa kuzaa hadi watoto ishirini kwa wakati mmoja. Panya wa aina hii hushambulia mazao ya nafaka, mazao ya mizizi, mazao jamii ya kunde pamoja na zao la pamba ambapo mashambulizi yake huanzia kwa mbegu zilizopandwa, miche, mazao yaliyokomaa shambani hadi yale yaliyohifadhiwa ghalani.

 

panya wa shambani
panya wa shambani

 

  1. Panya wa Darini (Rattus rattus)

Hii ni aina ya panya waharibifu wanaoishi majumbani ambao hupendelea sana kukaa katika paa la nyumba na kama ilivyo kwa panya shamba aina hii ya panya hupatikana karibu mikoa yote ya Tanzania na huweza kushambulia mazao yaliyo ghalani kama vile nafaka, mihogo, viazi, maharage, pamba na karanga.

 

  1. Aina nyingine za Panya

Aina nyingine za panya waharibifu ni panya mbilikimo wanaopendelea kuishi ndani ya nyumba au maghala na wakati mwingine hutoka nje kutafuta chakula. Mbali na panya shamba, panya wengine wanaovamia mashamba na kuharibifu mazao ni panya michanga na panya miraba.

 

Mahitaji Ya Msingi Ya Panya

Kwa kawaida panya kama ilivyo kwa wanyama wengine wana mahitaji makubwa manne muhimu ambayo wanapoyapata kwa urahisi katika sehemu fulani huweza kukua, kuzaliana na kuongezeka kwa kasi katika sehemu hiyo. Mahitaji hayo ni kama vile;

  1. Chakula,
  2. Maji,
  3. Maficho salama kwao pamoja na
  4. Sehemu ya kuzaliana.

 

Tabia Muhimu Za Panya

Kuna usemi unaosema, “Kumjua adui mapema kabla ya kupambana nae ni hatua mojawapo ya kupata ushindi.” Hivyo basi tuna kila sababu ya kutakiwa kumjua panya na tabia zake kabla hatujaanza kumdhibiti, zifuatazo ni baadhi ya tabia muhimu za panya;

  1. Panya ni wanyama wanaofanya shughuli zao nyingi wakati wa usiku (Nocturnal) na hupendelea kuishi maeneo yaliyojificha kama vile vichaka vya majani, mapori na katika mashimo ardhini wakiwa katika makundi tofauti yenye mipaka inayotambulika (territories) ambapo panya walio katika kundi moja hutambuana kwa njia ya kunusana. Kwa sababu hiyo katika eneo moja ni kitu cha kawaida sana kukuta kuna maficho mawili ya panya au zaidi katika sehemu tofauti.
  2. Panya hupendelea kula vyakula vyenye Protini na Vitamini kwa wingi na ndio maana kwa upande wa mbegu hupendelea sana kula sehemu ya kiini ya mbegu (embryo) na kuacha sehemu kubwa ya mbegu kama mabaki. Wanapokosa mazao ya kula shambani panya huweza kuishi kwa kula mijusi, konokono, vyura na wanyama wengine wadogo. Inakadiliwa kuwa panya mmoja kwa siku ana uwezo wa kula karibia asilimia 10 ya uzito wake sawa na gramu 25 za chakula kwa panya mkubwa.
  3. Panya wana uwezo mkubwa wa kuzaliana na idadi yao kuongezeka maradufu ndani ya kipindi cha muda mfupi ambapo panya jike mmoja huhitaji siku 60 hadi 70 kupevuka na kuanza kuzaa kutegemeana na uwepo wa chakula na maji. Kwa kawaida panya jike hubeba mimba kwa muda wa siku 21 kabla ya kuzaa idadi ya watoto wa tano hadi kumi kwa uzao mmoja ambapo inakadiliwa kuwa kuua panya jike mmoja kabla ya kuzaa ni sawa sawa na kuua panya 35 kabla ya kukomaa kwa mazao shambani. (Kwa ujumla tabia hii (iii) huwa na utofauti mdogo kutegemeana na aina ya panya, hali ya hewa na mazingira ya eneo husika).
  4. Panya wana uwezo mkubwa wa kuchimba mashimo ardhini ambapo kwa kutumia meno ya mbele na kucha za miguu huchimba na kutengeneza mfumo wa njia za chini kwa chini zinazoweza kuenea katika eneo la mita 25 au zaidi kuzunguka tundu la shimo.
  5. Panya wana uwezo mkubwa wa kukimbia ambapo kwa usiku mmoja tu panya wana uwezo kukimbia hadi umbali wa kilomita moja kutafuta chakula na hivyo kuvamia mashamba mbalimbali ya mazao.
  6. Panya wana uwezo mkubwa wa kunusa na kufuata harufu ya chakula hadi kufikia sehemu kilipo chakula na kwa sababu hiyo hawategemei sana macho yao katika utafutaji wa chakula wakati wa usiku.
  7. Panya wana uwezo mkubwa wa kuhisi joto na ndio maana hupendelea kutembea wakati wa usiku, asubuhi na jioni pindi joto linapokuwa chini na ikitokea ukamuona panya yoyote wakati wa mchana, hii ni ishara kuwa idadi yao imeshakuwa kubwa katika eneo husika.
  8. Panya wana uwezo mkubwa wa kusikia zaidi ya binadamu na hushtushwa na kelele yoyote ya ghafla.
  9. Panya wana uwezo mkubwa wa kukwea na kupanda juu ya miti hivyo ni rahisi sana kwao kupanda juu ya mashina ya mimea iliyopo shambani na kushambulia mazao kama vile mahindinyanya na alizeti.
  10. Panya wana tabia ya kutilia shaka na kuchukua taadhari juu ya kitu chochote kipya katika mazingira yao na kwa kawaida huwachukua takribani siku 4 hadi 5 kukizoea. Tabia hii ambayo kitaalamu hutambulika kama Neophobia ni muhimu sana kuizingatia hasa wakati wa kuwategea panya mitego na chambo.
  11. Panya wana uwezo wa kuishi unaotofautiana kati ya aina na aina lakini kwa upande wa panya shamba (Shamba rat) inakadiliwa ana uwezo wa kuishi wastani wa miezi 18.
  12. Panya wana tabia ya kuguguna vitu mbali mbali kama vile mbao, maganda ya nyaya na Aluminiamu ili kunoa meno yao ya mbele yenye tabia ya kukua bila kikomo kwa kipindi chote cha maisha yao.
  13. Panya wana uwezo mkubwa wa kuogelea na hivyo wana uwezo wa kutembea kwenye mazingira tofauti.
  14. Panya wana uwezo mdogo wa kuona ambapo uwezo wao wa kuona ni umbali wa mita kumi tu huku wakiwa hawana uwezo wa kutofautisha rangi kwani kila kitu kwao huonekana cha rangi ya kijivu.

 

Madhara Yanayosababishwa Na Panya

Panya wasipodhibitiwa huweza kumsababishia mkulima hasara kubwa kwa sababu wana uwezo wa kula mazao wakati yakiwa shambani na kufukua mashimo na kula mbegu za mazao zilizopandwa. Vilevile panya wana uwezo wa kula mazao yaliyoifadhiwa katika maghala na hivyo kusababisha hasara kubwa kwa mkulima ikiwa hatochukua hatua za kuwadhibiti mapema. Kwa kawaida panya hupendelea sana kula;

  1. Mazao ya nafaka kama vile mahindimpunga na mtama,
  2. Mazao ya mizizi kama vile mihogo na viazi,
  3. Mazao ya mafuta kama vile alizeti na karanga,
  4. Mazao jamii ya kunde kama vile mbaazi, maharage na kunde,
  5. Mazao ya mboga kama vile nyanya na matango,
  6. Mbegu za mazao ya mboga kama vile matikiti, maboga n.k.

Madhara mengine yanayoweza kusababishwa na panya ni pamoja na kueneza magonjwa mbalimbali kwa mifugo na kwa binadamu ambapo kwa binadamu pekeyake panya kwa aina zake tofauti wana uwezo wa kusababisha magonjwa karibia 50 kama vile ugonjwa wa Tauni, typhoid, paratyphoid n.k. Baadhi ya magonjwa hayo huenezwa kwa kupitia vinyesi na mikojo ya panya, panya kunusa au kulamba vyombo vya jikoni au kupitia utitiri na viroboto wa panya wanaoweza kuwauma wanyama na binadamu. Vilevile panya wanaweza kusababisha uharibifu mkubwa kwa vitu mbalimbali majumbani kama vile kutoboa makabati, kutafuna nguo, pamoja na nyaya za umeme.

 

MLIPUKO WA PANYA

Kwa kawaida mashambulizi ya panya katika mashamba hutokea kwa mlipuko katika vipindi au majira fulani ambapo mara nyingi kwa upande wa Tanzania panya huvamia maeneo ya mashamba na kuanza kula mazao wakati wa kipindi cha mvua hasa kipindi cha masika au wakati mwingine ndani ya kipindi cha mvua za vuli. Kwa mfano kwa mkoa wa Morogoro mlipuko wa panya mara nyingi hutokea muda wowote kuanzia mwezi Machi hadi Mei na kuendelea hadi mwezi Septemba mwanzoni mwa mvua za vuli na hivyo kusababisha hasara kwa wakulima katika eneo kubwa ngazi ya bonde la kilimo, kijiji, Kata au hata Wilaya.

Hivi karibuni mkoani Morogoro mwishoni mwa mwaka 2017 hadi mwanzoni mwa mwaka 2018 katika maeneo ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero na Halmashauri ya mji mdogo wa Ifakara kuliripotiwa kuwepo kwa mlipuko wa panya ambapo takribani zaidi ya ekari 350 za mahindi na mpunga ziliharibiwa kufuatia uvamizi wa panya mashambani na kula mazao. Maeneo yaliyoathiriwa kwa upande wa Wilaya ya Kilombero ni pamoja na Tarafa ya Mngeta katika kata za Melela, Mwaya na Chita na vilevile vijiji vya Ihanga, Lumuma na Idete kwa upande wa Halmashauri ya Mji mdogo wa Ifakara.

 

Ukaguzi Wa Shamba

Kabla ya kuelezea ni mbinu gani utumie katika kukabiliana na mlipuko au uvamizi wa panya katika shamba lako ningependa ujue kuwa kufanya ukaguzi wa shamba ni sehemu muhimu sana katika udhibiti wa panya kwani kwa kufanya ukaguzi unaweza kutambua uwepo wa panya katika shamba lako, maficho yao na chanzo cha tatizo ili kuweza kuchukua hatua stahiki.

Ukizingatia tabia ya panya kupenda kuishi kwa makundi katika sehemu tofauti za eneo moja fanya ukaguzi katika sehemu zote za shamba lako kati, pembezo na maeneo mengine yote ya karibu na shamba na endapo utabaini maficho ya panya sehemu fulani hakikisha unaendelea na ukaguzi hadi utakapokamilika kwani kuna uwezekano mkubwa wa uwepo wa maficho ya panya sehemu nyingine. Kama ilivyoelezwa katika sehemu ya tabia za panya kwa kawaida mashambulizi ya panya ni matokeo ya panya walio katika maficho mawili au zaidi katika eneo moja hivyo maeneo yote ndani ya shamba na karibu na shamba yana umuhimu sawa katika zoezi la ukaguzi. Kwa mantiki hiyo zoezi hili ni busara likahusisha jamii nzima kwa eneo husika ili kuongeza ufanisi.

Inashauriwa ukaguzi wa shamba ufanyike mara kwa mara ili kuweza kubaini mapema uwepo wa panya kabla idadi yao haijawa kubwa ambapo kwa upande wa muda unaofaa kufanya ukaguzi ili kuwaona panya kwa urahisi katika shamba lako ni wakati wa asubuhi, jioni au usiku kwa kutumia tochi kama ukiweza. Muda huu ndio ambao panya hupendelea kutembea na kula mazao katika mashamba. Wakati wa kufanya ukaguzi katika shamba lako ni vyema kuzingatia viashiria vya uwepo wa panya vinavyoweza kuonekana.

 

Vishiria vya Uwepo wa Panya katika shamba

Uwepo wa panya katika shamba au mahali popote huwa na viashiria vinavyoonekana kutokana na shughuli za panya katika eneo husika. Ni muhimu sana kuvijua viashiria hivi kwani vinaweza kukusaidia wakati unapofanya ukaguzi wa shamba. Wakati mwingine kiashiria kimoja kinaweza kisikupe majibu sahihi juu ya uwezekano wa kuwepo uvamizi wa panya katika shamba lako hivyo ni busara kuzingatia viashiria zaidi ya kimoja kabla ya kusema shamba limevamiwa au la. Unapoona kuna viashiria vifuatavyo katika shamba lako jua ya kuwa kuna uwezekano mkubwa wa uwepo wa panya.

 

  • Panya wazima au mizoga

Panya wazima wanaweza kuonekana kwa urahisi ikiwa utafanya ukaguzi wakati ambao wao hupendelea kutembea kama ilivyoelezwa hapo juu. Kwa makadilio ukimwona panya mmoja awe mzima au amekufa katika shamba ujue kuna uwezekano wa kuwepo panya wengine 25 au zaidi ambao bado haujawaona.

 

  • Mazao yaliyoshambuliwa na panya

Mazao yaliyoshambuliwa na panya katika shamba lako ni ishara tosha ya uwezekano wa kuwepo kwa panya shambani kwa mfano, katika bustani ya nyanya unaweza kukuta mabaki ya nyanya zilizoliwa au kukuta mahindi yamegugunwa kutoka katika magunzi yakiwa shambani.  Vilevile mabaki ya mbegu zilizoliwa kiini kwa mazao mbalimbali ya nafaka kama vile mahindi na mashina ya mimea yaliyoliwa kama vile mashina ya miwa ni ishara kuwa mazao hayo yameshambuliwa na panya.

 

  • Vinyesi na madoa ya mikojo ya panya

Kwa kawaida vinyesi vya panya vina ukubwa tofauti kutegemeana na aina ya panya lakini ukubwa wake unalingana kwa karibu na ukubwa wa punje moja ya mchele hadi mbegu moja ya maharage. Vinyesi vya panya kwa aina za panya karibu zote vinapokuwa vibichi huonekana vyenye unyevu na rangi ya kung’aa lakini vinapokauka hubadilika rangi na kuwa na rangi nyeusi.

Michirizi ya mikojo na vinyesi vya panya vinaweza kuonekana katika sehemu tofauti ndani ya mipaka ya makundi ya panya hasa katika njia zao na kwa maeneo utakayokuta idadi kubwa ya vinyesi vya panya ujue maeneo hayo ndiyo wanayopendelea zaidi kuyatembelea. Vilevile kwa kufuatilia michirizi ya mikojo na vinyesi vya panya unaweza kugundua kwa urahisi njia za panya na maficho yao.

 

 
  • Njia za panya

Panya kwa kawaida wanapovamia eneo fulani hutengeneza njia zao ambazo huzitumia mara kwa mara wakati wanapotafuta mahitaji yao mbalimbali. Njia hizi mara nyingi huelekea hadi yalipo maficho yao na hivyo wakati wakufanya ukaguzi unaweza kufuata njia hizi na kuweza kubaini maficho ya panya wanaoshambulia mazao katika shamba lako.

 

  • Alama za nyayo za panya.

Panya huweza kuacha alama za nyayo zao katika ardhi wanapotembea kutoka sehemu moja kwenda nyingine wakati wa kutafuta mahitaji yao. Nyayo hizi unaweza kuziona katika sehemu ya shamba yenye mazao yaliyoshambuliwa au katika njia za panya. Katika mashamba yasiyo na magugu au yenye magugu mafupi unaweza kutumia alama za nyayo ili kubaini njia za panya na maficho yao.

 

 Mashimo au maficho ya panya

Kama ilivyoelezwa katika sehemu ya tabia za panya kwamba panya hupendelea kuishi katika maeneo yaliyojificha ili kujikinga na maadui (predators) na kuweza kuzaliana kwa usalama kuwepo kwa mashimo au maficho ya panya sehemu yoyote ndani au maeneo ya karibu na shamba ni ishara wazi kwamba katika eneo hilo kuna uvamizi wa panya.

 

Panya akichungulia kutoka katika shimo
Panya akichungulia kutoka katika shimo

 

  • Mashimo yaliyopandwa mbegu kufukuliwa

Panya kama nilivyokuelezea hapo awali wana uwezo wa kufukua mashimo yaliyopandwa mbegu za mazao mbalimbali na kula mbegu hizo hata kabla ya kuota. Hivyo unapokuta mashimo yamefukuliwa na mbegu kuliwa kabla ya kuota jua ya kuwa shamba lako limevamiwa na panya.

 

  • Milio ya panya

Panya wana uwezo wa kutoa sauti kali ya milio inayoweza kusikika hadi kufikia umbali mrefu kidogo. Kwa sababu hiyo unaposikia milio ya panya katika sehemu tofauti katika shamba lako au maeneo mengine elewa kuwa kuna uwezekano wa kuwepo kwa panya mahali hapo.

Comments

Popular Posts