Thursday, October 12, 2023

Jinsi ya kufanya Kilimo Bora cha Karoti

 

Karoti ni Nini?

Karoti kwa jina la kisayansi inajulikana kama Daucus carota. Ni miongoni mwa mazao kadhaa ya bustani (mbogamboga) yenye thamani kubwa kwa sasa hapa nchini na duniani kote.

Kilimo cha karoti huhitaji uangalizi mdogo sana hivyo kuifanya kuwa miongoni mwa mazao yanayoweza kusimamiwa hata na mtu ambaye ana shughuli nyingi nyinginezo ukilinganisha na mazao mengine ya mboga mboga.

Zao la karoti ni zao la jamii ya mzizi, kwa kawaida hupatikana katika rangi ya machungwa, zambarau, nyeusi, nyekundu, nyeupe na njano. Karoti ni aina ya mboga yenye vyanzo vingi vya calcium, iron na wingi wa vitamin B.

Zao hili linalimwa maeneo mengi sana nchini ikiwa pamoja na Mbeya, Morogoro (maeneo ya Uluguru na Mgeta), Iringa, Kilimanjaro na  Kagera.



Aina Za Karoti Zinazolimwa Hapa Tanzania

  • Nantes

Aina hii inapatikana maeneo mengi na inalimwa sana hapa Tanzania. Inakuwa kwa haraka na inapendwa na watu kutafunwa kwani ladha yake ni tamu sana.

  • Chantenay Red Core

Hii pia ina ladha nzuri nainataka kufanana na Nantes lakini mizizi yake ni dhaifu ukilinganisha na Nantes.

  • Oxheart

Karoti za Oxheart ni  fupi  na nene. Huvunwa baada ya muda mfupi kulinganisha na aina zingine.


kilimo cha karoti
Karoti safi baada ya kuvuna

Hali Ya Hewa Inayofaa Kwa Kilimo Cha Karoti

Karoti  inastawi  katika  hali joto la wastani  kuanzia  nyuzi  joto  15  hadi  20 sentigredi, japokuwa  inaweza  kustahimili  katika  nyuzi  joto  27.  Karoti haiitaji  baridi sana wala joto sana.


Mahitaji Ya Udongo Kwa Kilimo Cha Karoti

Karoti inahitaji udongo  wenye  tindikali  kuanzia  PH  5.5-6.8, udongo  wa  kichanga na  laini (Kichanga  chepesi)  unaoruhusu  hewa  na  maji  kupita  bila  kutuama. Udongo ukiwa wa kichanga kizito na kama unatuamisha maji hufanya mizizi kuwa dhaifu sana au midogo pia maji kutuama kunasababisha  mizizi  kuoza.


Namna Ya Kutayarisha Shamba

Katika kilimo cha karoti, ili kupata mavuno mengi na bora, eneo la kupanda halina budi kutayarishwa vizuri. Iwapo shamba ni jipya, miti, magugu na visiki vyote vikatwe. Visiki na takataka zote ziondolewe shambani.

Baada ya hapo shamba linahitaji kutifuliwa vizuri na katika kina cha kutosha kuanzia sentimita 30 hadi 45. Lainisha udongo ili kurahisisha uotaji wa mbegu za karoti ambazo ni ndogo sana.

Kama eneo lina udongo wa mfinyanzi au wa kichanga ni muhimu kuweka mbolea za asili zilizooza vizuri. Mbolea hizi hufanya udongo wa mfinyanzi uwe mwepesi au kuwa na umbo zuri kuweza kuruhusu maji na hewa kupenya kwa urahisi.

Endapo karoti zitastawishwa wakati wa mvua nyingi zipandwe kwenye matuta yaliyoinuliwa  kwa  mwinuko  wa  sentimita 28  hadi 40 ili  kuzuia maji  kutuama  na kusababisha  mizizi  kuoza au  kuto kukua  vizuri.


Uoteshaji Wa Karoti

Karoti hupandwa kwa kutumia mbegu moja kwa moja shambani bila kupandikiza, kiasi cha mbegu kinachotumika kupanda ni 3.5 – 4 kg kwa ekari. Mstari mmoja hadi mwingine ni sentimita 30 na  mche mmoja hadi mwingine ni sentimita 10. Ila pia inaweza kubadilika kulingana na aina ya karoti.

Kwa kawaida hairuhusiwi kuhamisha miche kwa sababu mizizi yake ni dhaifu ambayo haitastahimili kukua baada ya kuhamishwa. Baada ya wiki ya nne kutoka kupandwa inatakiwa kung’olea miche iliyorundikana ili kuipa nafasi kwaajili ya kufanya miche iwe na afya nzuri.


Mahitaji Ya Maji / Umwagiliaji

Hakikisha udongo wako una unyevu muda mwingi. Kama sio kipindi cha mvua, basi ujitahidi kumwagilia angalau mara mbili au mara tatu kwa wiki ili udongo upate unyevu wa kutosha. Karoti  ikikosa  maji  huzaa  mizizi  midogo  ambayo  ni  dhaifu  sana,  na  udongo  mkavu  ukipata  maji  mengi  gafla  husababisha  karoti  kupasuka,  hivyo  hakikisha  udongo  wako  unakuwa  na  unyevu  muda  wote.


Mahitaji Ya Mbolea kwa Karoti

Tumia mbolea ya DAP wakati wa kupanda, CAN ama SA 100kg wiki tatu baadaye na kisha tumia NPK wiki sita baada ya kupanda. Matumizi ya mbolea za maji yafanyike kila baada ya wiki mbili kutegemea na mahitaji, kisha tumia NPK wiki sita baada ya kupanda.

NPK inayotumika iwe na kiwango kidogo cha Nitrojeni (N) ila kiwango cha phosphate (P) na potasiamu (K) kiwe kikubwa kwa ajili ya kufanya mizizi ya karoti kuwa vizuri. Mbolea ikizidi sana katika karoti inasabibisha kuwa na  ladha mbaya pia karoti ina kuwa na vimizizi vidogo kama vinyweleo hivyo kupunguza ubora wa karoti.


Kudhibiti Magugu

Palilia shamba mara kwa mara ili kuhakikisha shamba halina magugu. Magugu hudhibitiwa kwa palizi ya jembe, kung’oa kwa mkono ama matumizi ya viuagugu. Matumizi ya viuatilifu yafanyike kila baada ya wiki mbili


Magonjwa Sumbufu ya zao la Karoti

(i) Madoa jani (Leaf Spot)

Ugonjwa huu husababishwa na ukungu na hutokea wakati karoti zina urefu wa sentimita 13 mpaka 15. Hushambulia majani na kuyafanya yawe na madoa yenye rangi nyeusi iliyochanganyika na kijivu au kahawia. Sehemu zinazozunguka madoa haya hubadilika rangi na kuwa njano. Ugonjwa ukizidi majani hukauka.

Zuia ugonjwa huu kwa kunyunyizia dawa za ukungu kama vile Dithane – M 45, Blitox, Copperhydroxide (Kocide), Copper Oxychloride, Cupric Hydroxide (Champion), Antrocol, Topsin M- 70% na Ridomil.

(ii) Magonjwa ya bacteria (bacterial disease).

Huu ugonjwa husababisha kusinyaa kwa mimea (wilting), na kufanya mmea usikue (stunted growth) na shina kuoza (stem rot) pamoja na kuoza kwa karoti.

(iii) Kuoza Mizizi (Sclerotinia Rot)

Ugonjwa huu husababishwa na ukungu na hushambulia mizizi namajani. Dalili zake ni kuoza kwa mizizi na majani. Baadaye sehemu hizi hufunikwa na uyoga mweupe. Kwenye uyoga huu huota siklerotia kubwa zenye rangi nyeusi.

Zuia ugonjwa huu kwa kuzingatiayafuatayo:
a) Epuka kustawisha karoti kwenye maeneo yaliyoshambuliwa na ugonjwa huu.
b) 
Nyunyuzia dawa za ukungu kama vileDithane M- 45, Blitox, Topsin – M 70% na Ridomil.

(iv) Magonjwa ya fangasi (fungal disease) 

kama kata kiuno (damping off) huu ugonjwa hushambulia sana miche hufanya miche ishindwe kukua vizuri na mara nyingi hupelekea mche kufa.


Wadudu Wasumbufu wa Zao la Karoti

i) Minyoo Fundo:

Minyoo hii hushambulia mizizi na kuifanya iwe na vinundu. Hali hii husababisha mmea kudumaa na kupunguza mavuno. Minyoo fundo huweza kuzuiwa kwa kubalidilisha mazao. Baada ya kuvuna usipande mazao ya jamii ya karoti au mazao yanayoshambuliwa na wadudu hawa. Unaweza kupanda mazao ambayo hayashambuliwi na minyoo fundo kama vile mahindi. Pia hakikisha shamba ni safi wakati wote.

ii) Imi wa Karoti

Mashambulizi hufanywa na funza ambaye hutoboa mizizi. Ili kuzuia wadudu hawa tumia dawa kama vile Dichlorvos, Sapa Diazinon na Fenvalerate. Pia badilisha mazao na wakati wa kupalilia pandishia udongo kufunika mizizi.

iii) Karoti Kuwa na Mizizi Mingi (Folking)

Hii hutokea kama karoti zimepandwa kwenye udongo wenye takataka nyingi na usiolainishwa vizuri. Vile vile utumiaji wa mbolea za asili zisizooza vizuri unaweza kusababisba karoti kuwa na mizizi mingi. Hali hii inaweza kuzuiwa kwa kulainisha udongo vizuri na kutumia mbolea za asili zilizooza vizuri.


Jinsi ya Kuvuna Na Kuhifadhi Karoti

Karoti   huvunwa  baada  ya  miezi  mitatu  toka  kupanda  au  kuanzia  wiki  11   hadi  13  kulingana  na  hali  ya  hewa  ya  eneo  ilipolimwa. Karoti  huvunwa  kwa  kung’oa  miche  yake  na  kuchukua mizizi  yake  ambayo  ndiyo  inayotumika  kama  kiungo  katika  vyakula au katika  matumizi  mengine  kama  dawa.

uvunaji wa karoti
Uvunaji wa karoti

Mavuno  ya  karoti  kwa  ekari  moja  ni  kuanzia   tani  10  hadi  15, endapo  utalima  kitaalam (kwa  kutumia  technolojia  za  kilimo  kama   mbegumboleaviuatilifu).

Baada ya  kuvuna  kama  hutauza  hapo hapo hifadhi kwenye baridi ya nyuzi joto moja hadi 4 unaweza hifadhi karoti kwa zaidi ya wiki kabla hujaziuza. Jitahidi upate coldroom hata ya mita tatu kwa tatu ili kujiepushia hasara.


Soko La Karoti

Soko la karoti lipo lina patikana kwa uhakika, kwa sababu karoti inatumika kama kiungo (spice) katika vyakula kama  nyama, wali au  pilau  na vyakula vingine.

Watu wengi hupendelea karoti kutokana na umuhimu wake katika lishe, kwa hiyo soko hupatikana katika mikoa yote Tanzania. Karoti moja inauzwa kuanzia shilingi 100 hadi 200 kulingana na upatikanaji wake eneo  husika. Pia hupimwa kwa kilo kuanzia shilingi 1,000.

Wadudu waharibifu wa nyanya na dawa zake

 Ili uweze kubaini mapema uwepo wa wadudu waharibifu au magonjwa katika mimiea yako ya nyanya ni lazima uwe unachunguza mimea yako mara kwa mara. Angalia uwepo wa wadudu kwenye sehemu ya chini ya majani, juu yake, kwenye mashina, maua au matunda kama yametobolewa au la.

 

Sasa ungana nami katika makala hii uweze kujua ni wadudu wepi waharibifu kwenye zao lako la nyanya shambani kwako ili uweze kukabiliana nao. Pia waweza kujua magonjwa ya nyanya na dawa zake hapa

 

1. Funza wa vitumba: American bollworm (Helicoverpa armigera)

Kubaini mapema mayai au funza kabla hayajatoboa matunda ni muhimu sana. Funza wachanga kwanza hula majani baadae matunda. Funza wakishaingia ndani ya matunda husababisha uharibifu mkubwa. Uharibifu kwenye matunda machanga husababisha kupukutika kwake, wakati mashambulizi ya matunda yaliyokomaa husababisha matundu ambayo huruhusu kuingia kwa aina nyingine za ukungu na bakteria ambao huleta madhara zaidi.

 

funza-wa-vitumba-anavyotoboa-matunda-ya-nyanya
Funza wa vitumba anavyotoboa nyanya

 

 

Kipepeo chake huwa na rangi ya manjano-kahawia chenye doti iliyokoza, mistari isiyo sawa ya kijivujivu na alama nyeusi yenye umbile la figo kwenye mbawa za mbele. Mbawa za nyuma ni nyeupe na baka jeusi katika sehemu za nje. Kipepeo huwa na urefu wa 14-18mm na upana wa mbawa wa 35-40mm.

Namna ya kudhibiti

Kubainika mapema hupatikana kwa kuchunguza mazao kila mara. Angalia majani yaliyo chini ya maua ya juu yaliyochanua kwa kutafuta mayai ya viwavi tumba/dukari. Baada ya kubainika kwa funza huyu fuata mbinu zifuatazo:

Mbinu bora za kilimo

•Chuma na teketeza matunda yaliyoathirika.

•Ondoa na teketeza mabaki ya mazao baada ya kuvuna.

•Chimbulia ardhi baada ya mavuno.

•Fanya mzunguko wa mazao.

•Toa kwa mkono na teketeza mayai na funza wadogo wadogo.

•Epuka kupanda nyanya karibu na pamba au mahindi.

•Changanya mazao, panda na pilipili na maua bange (African marigold).

Dawa (Chemical control)

Mara nyingi dawa (kemikali) inayodumu kwa muda mfupi ndio inayohitajika kwani matunda hushambuliwa muda mfupi kabla ya kuvuna. Kwa hivyo, dawa kama vile mevinphos na endosulfan zinashauriwa kutumika. Dawa nyingine zilizosajiliwa kutumika kwa mdudu huyu ni carbaryl, tetrachlorvinphos, methomyl, acephate, monocrotophos na dawa zenye pareto.

Kibaiolojia (Biological control)

Funza wa vitumba wana maadui wengi asilia wakiwemo viumbe wanaokula mayai (kama Trichogramma spp.), wanaoshambulia funza (nyigu na nzi wanaokula funza) na washambulizi kama vile aina za maji moto, assassin bugs, minute pirate (anthocorid) bugs, lacewings na ladybird beetles. Kuku na ndege pia hula mafunza na mabuu wakati fulani katika ukuaji wa matunda. Madawa ya kibaiolojia hujumuisha Muarobaini (Azadirachta indica) na Bt (Bacillus thuringiensis). Madawa yatokanayo na Bt yanayouzwa kwa udhibiti wa mafunza hujumuisha Dipel, Thuricide (zote ni aina za Bt kurstaki), Florbac 70 DG na XenTari (zote ni aina za Bt aizawai).

 

Yafahamu magonjwa hatari ya nyanya na jinsi ya kukabiliana nayo

2. Utitiri Mwekundu: Red spider mites  (Tetranychus urticae)

Utitiri wekundu huwa ni tatizo hasa wakati wa kiangazi. Utitiri huu unaweza kutambulika kwa kutumia lenzi ya mkono. Dalili za awali hujumuisha madoa ya manjano, ambayo hujitokeza pale mashambulizi yanapokuwa makubwa; baada ya hapo njano kubwa na ishara za kama kuungua hujitokeza kwenye majani na matunda ikifuatiwa na utando kama wa buibui.

 

Utitiri-mwekundu-wa-nyanya-ulivyotanda-kwenye-jani-la-nyanya
Utitiri mwekundu

 

Mashambulizi makubwa husababisha umanjano wa majani na matunda, kupukutika mapema kwa majani, kukauka kwa mti kuanzia kileleni na kufa kwa mmea. Vichungu vya utitiri wekundu hujikusanya kwenye ncha za majani wakati idadi ya utitiri wekundu inapozidi chakula kilichopo.

Namna ya kudhibiti

Fanya uangalifu wa kubaini utitiri wekundu kwenye mazao na chukua hatua mara unapowabaini. Matumizi ya dawa muafaka haraka pale tu utitiri wekundu wanapobainika, husaidia kupunguza athari.

Mbinu bora za kilimo

•Weka matandazo na mwagilia

•Ngo’a na choma moto mimea iliyoathirika

•Choma moto mabaki yote ya mazao baada ya kuvuna

•Fanya mchanganyiko wa mazao na vitunguu maji au vitunguu swaumu

Dawa (Chemical control)

Tumia dawa za kemikali pale tu utakapowabaini, na baada ya hapo tumia dawa za aina mbali mbali kwa kupishana kuzuia usugu wa utitiri wekundu. Aina nyingi za madawa zinaweza kutumika, kama vile Dimethoate, Abamectin, Bifenthrin na acephate.

Kibaiolojia (Biological control)

Aina ya utitiri shambulizi ni adui asilia wa utitiri wekundu anayepatikana kwenye maduka yanayouza viumbe washambulizi kwa matumizi kwenye jengo la kuoteshea mimea na hufanya kazi vizuri wanapodhibitiwa vyema. Hii inahitaji udhibiti mzuri bila ya kutumia madawa ya kemikali ya kuulia wadudu. Matumizi ya dawa za kemikali za kuulia wadudu zinaweza zikasababisha kutofanya kazi vizuri kwa viumbe hawa kwani wadudu wanaokula chawa wekundu huuliwa na dawa hizi.

3. Minyoo Fundo: Root knot nematodes (Meloidogyne spp.)

Dalili za minyoo fundo hujumuisha kupiga umanjano na kudumaa kwa mimea na hatimaye kunyauka wakati wa jua kali. Mimea iliyoathirika hujitokeza shambani kwa sehemu sehemu. Mashambulizi husababisha kupungua kwa mazao ikitegemea ukubwa wa mashambulizi kwenye mizizi, mashambulizi makubwa husababisha kufa kwa mimea. Mimea huwa na stahimili ndogo kwa magonjwa mengine.

 

Minyoo-fundo-kwenye-mizizi-ya-nyanya
Minyoo fundo

 

Mimea inapong’olewa kutoka kwenye udongo, mizizi huonekana imevimba yenye maumbile mabaya na vifundo, yanayojulikana kama mafundo ya mizizi. Ukubwa wa vifundo hivi unaweza kuwa sawa na ukubwa wa kichwa cha pini ya kirungu mpaka 25mm au zaidi. Mashambulizi makubwa husababisha mzizi wote ukawa na umbile baya na mafundo ambao hatimaye huoza. Mashambulizi yanayofuata husababisha uharibifu na dalili za magonjwa huongezeka kwenye nyanya.

Namna ya kudhibiti

Mimea mingi inayopandwa huwa na minyoo fundo. Minyoo huweza kuingizwa shambani kupitia miche kutoka vitaluni au kwa usambaaji kutoka shamba hadi shamba katika maeneo yenye mashambulizi. Hatua zifuatazo zinaweza kuchukuliwa ili kudhibiti minyoo ya mimea.

Mbinu bora za kilimo

•Tumia mimea ya mitego kama vile Mbange ‘marigold’ (Tagetes spp.) na haradali ya India.

•Dumisha kiwango kikubwa cha mbolea za asili (samadi na mboji) katika udongo.

•Changanya mashudu (mabaki) ya muarobaini na udongo.

•Tumia aina zenye kustahimili minyoo fundo (kama Caracas, Kentom, Meru, Piersol, Roma VFN, Tengeru 97, Zest F1, Star 9001 na Star 9003).

•Zungusha mazao na vitunguu majimahindi madogo, mahindi matamu, mahindi, mtama, uwele, ufuta, au nyasi. Mbinu ya mzunguko wa mazao unaojulikana kama “STRong” unashauriwa kutumika katika udhibiti wa minyoo fundo. Mbinu hii inashauri kupandwa kwa mmea usiostahimili (kama Nyanya), ikifuatiwa na zao lenye kustahimili kidogo (kama Kebeji), halafu zao lenye kustahimili kabisa (kama Vitunguu maji), kabla ya kurejea tena zao lisilostahimili (kama Nyanya).

•Ng’oa mizizi na uchome moto mimea iliyoathirika na takataka zote za mazao.

•Ua vimelea vya maradhi kwenye vitalu kwa kutumia moto au mvuke kabla ya kusia mbegu.

•Epuka kupandikiza miche iliyoathirika.

•Tumia mbinu za kibaiolojia kwa kutumia bidhaa zinazotokana na Trichoderma.

Dawa (Chemical control)

Minyoo fundo inaweza kudhibitiwa kwa kutumia dawa ya minyoo/wadudu (Vydate L) na dawa za kufukiza (Telone II, Telone C-17, Vapam), lakini hizi hazipatikani kwa urahisi.

Kibaiolojia (Biological control)

Udhibiti wa kibaiolojia unahusisha matumizi ya viumbe wapinzani wa minyoo fundo (kama ukungu na bacteria). Kuna aina nyingi za ukungu zinazokula minyoo. Baadhi ya aina za ukungu (Arthrobotryts spp. na Monacrosporium spp.) hutumia nyuzi zao na mbegu zinazoganda kama mitego ya kunasia minyoo, aina nyingine za ukungu (kama Pochonia chlamydosporiaTrichoderma spp. na Paecilomyces lilacinus) hufyonza mayai na minyoo jike. Aina za bakteria maarufu wapinzani wa minyoo ni Pasteuria penetrans na Bacillus spp.

4. Sota (Cutworms)

Hushambulia miche ya nyanya hasa baada ya kupandikizwa shambani. Wakati wa mchana hujificha kwenye udongo na usiku hujitokeza na kukata miche kwenye shina usawa wa udongo.

 

Sota: wadudu waharibifu wa mimea ya nyanya

 

Namna ya kudhibiti

· Nyunyiza dawa za kuua wadudu (kama Rogor, Actellic, Selecron, Dursban) kwenye shina usawa wa udongo

· Hakikisha miche inapata maji ya kutosha

 

Yafahamu magonjwa hatari ya nyanya na jinsi ya kukabiliana nayo 

 

5. Vidukari au Wadudu mafuta (Aphids)

Ni wadudu wenye rangi nyeusi au kuijani au kahawia. Hukaa chini ya majani na kufyonza utomvu kwenye majani machanga. Hudumaza mmea na kushindwa kuzaa matunda

Aphids-wa-nyanya
Wadudu mafuta

 

Namna ya kudhibiti

Nyunyizia dawa za sumu za kuulia wadudu kama Rogor, Actellic, Selecron, Dursban maji ya majani ya mwarobaini na utupa, maji ya pilipili.

6. Inzi weupe (White flies)

Hawa ni Inzi weupe wadogo sana. Hujitokeza sana wakati wa kiangazi. Wadudu hawa hueneza ugonjwa wa nyanya wa virusi ujulikanao kama Rasta.

Whiteflies-kwenye-jani-la-nyanya
Nzi weupe kwenye jani la nyanya

 

Namna ya kudhibiti

Nyunyizia dawa za sumu za kuulia wadudu kama Selecron, Actellic, Dursban na thionex. Pia maji ya majani ya mwarobaini na utupa.

 

Haya sasa ni zamu yako, tuambie ni nini ulifanya ulipokumbana na wadudu kwenye shamba/bustani yako ya nyanya? je ulitumia dawa gani ambayo ungependa kumshauri mkulima mwenzako nae aitumie? Au bado wadudu wanaukusumbua shambani kwako? Acha comment yako hapa!