Jinsi ya kufanya Kilimo Bora cha Karoti

 

Karoti ni Nini?

Karoti kwa jina la kisayansi inajulikana kama Daucus carota. Ni miongoni mwa mazao kadhaa ya bustani (mbogamboga) yenye thamani kubwa kwa sasa hapa nchini na duniani kote.

Kilimo cha karoti huhitaji uangalizi mdogo sana hivyo kuifanya kuwa miongoni mwa mazao yanayoweza kusimamiwa hata na mtu ambaye ana shughuli nyingi nyinginezo ukilinganisha na mazao mengine ya mboga mboga.

Zao la karoti ni zao la jamii ya mzizi, kwa kawaida hupatikana katika rangi ya machungwa, zambarau, nyeusi, nyekundu, nyeupe na njano. Karoti ni aina ya mboga yenye vyanzo vingi vya calcium, iron na wingi wa vitamin B.

Zao hili linalimwa maeneo mengi sana nchini ikiwa pamoja na Mbeya, Morogoro (maeneo ya Uluguru na Mgeta), Iringa, Kilimanjaro na  Kagera.



Aina Za Karoti Zinazolimwa Hapa Tanzania

  • Nantes

Aina hii inapatikana maeneo mengi na inalimwa sana hapa Tanzania. Inakuwa kwa haraka na inapendwa na watu kutafunwa kwani ladha yake ni tamu sana.

  • Chantenay Red Core

Hii pia ina ladha nzuri nainataka kufanana na Nantes lakini mizizi yake ni dhaifu ukilinganisha na Nantes.

  • Oxheart

Karoti za Oxheart ni  fupi  na nene. Huvunwa baada ya muda mfupi kulinganisha na aina zingine.


kilimo cha karoti
Karoti safi baada ya kuvuna

Hali Ya Hewa Inayofaa Kwa Kilimo Cha Karoti

Karoti  inastawi  katika  hali joto la wastani  kuanzia  nyuzi  joto  15  hadi  20 sentigredi, japokuwa  inaweza  kustahimili  katika  nyuzi  joto  27.  Karoti haiitaji  baridi sana wala joto sana.


Mahitaji Ya Udongo Kwa Kilimo Cha Karoti

Karoti inahitaji udongo  wenye  tindikali  kuanzia  PH  5.5-6.8, udongo  wa  kichanga na  laini (Kichanga  chepesi)  unaoruhusu  hewa  na  maji  kupita  bila  kutuama. Udongo ukiwa wa kichanga kizito na kama unatuamisha maji hufanya mizizi kuwa dhaifu sana au midogo pia maji kutuama kunasababisha  mizizi  kuoza.


Namna Ya Kutayarisha Shamba

Katika kilimo cha karoti, ili kupata mavuno mengi na bora, eneo la kupanda halina budi kutayarishwa vizuri. Iwapo shamba ni jipya, miti, magugu na visiki vyote vikatwe. Visiki na takataka zote ziondolewe shambani.

Baada ya hapo shamba linahitaji kutifuliwa vizuri na katika kina cha kutosha kuanzia sentimita 30 hadi 45. Lainisha udongo ili kurahisisha uotaji wa mbegu za karoti ambazo ni ndogo sana.

Kama eneo lina udongo wa mfinyanzi au wa kichanga ni muhimu kuweka mbolea za asili zilizooza vizuri. Mbolea hizi hufanya udongo wa mfinyanzi uwe mwepesi au kuwa na umbo zuri kuweza kuruhusu maji na hewa kupenya kwa urahisi.

Endapo karoti zitastawishwa wakati wa mvua nyingi zipandwe kwenye matuta yaliyoinuliwa  kwa  mwinuko  wa  sentimita 28  hadi 40 ili  kuzuia maji  kutuama  na kusababisha  mizizi  kuoza au  kuto kukua  vizuri.


Uoteshaji Wa Karoti

Karoti hupandwa kwa kutumia mbegu moja kwa moja shambani bila kupandikiza, kiasi cha mbegu kinachotumika kupanda ni 3.5 – 4 kg kwa ekari. Mstari mmoja hadi mwingine ni sentimita 30 na  mche mmoja hadi mwingine ni sentimita 10. Ila pia inaweza kubadilika kulingana na aina ya karoti.

Kwa kawaida hairuhusiwi kuhamisha miche kwa sababu mizizi yake ni dhaifu ambayo haitastahimili kukua baada ya kuhamishwa. Baada ya wiki ya nne kutoka kupandwa inatakiwa kung’olea miche iliyorundikana ili kuipa nafasi kwaajili ya kufanya miche iwe na afya nzuri.


Mahitaji Ya Maji / Umwagiliaji

Hakikisha udongo wako una unyevu muda mwingi. Kama sio kipindi cha mvua, basi ujitahidi kumwagilia angalau mara mbili au mara tatu kwa wiki ili udongo upate unyevu wa kutosha. Karoti  ikikosa  maji  huzaa  mizizi  midogo  ambayo  ni  dhaifu  sana,  na  udongo  mkavu  ukipata  maji  mengi  gafla  husababisha  karoti  kupasuka,  hivyo  hakikisha  udongo  wako  unakuwa  na  unyevu  muda  wote.


Mahitaji Ya Mbolea kwa Karoti

Tumia mbolea ya DAP wakati wa kupanda, CAN ama SA 100kg wiki tatu baadaye na kisha tumia NPK wiki sita baada ya kupanda. Matumizi ya mbolea za maji yafanyike kila baada ya wiki mbili kutegemea na mahitaji, kisha tumia NPK wiki sita baada ya kupanda.

NPK inayotumika iwe na kiwango kidogo cha Nitrojeni (N) ila kiwango cha phosphate (P) na potasiamu (K) kiwe kikubwa kwa ajili ya kufanya mizizi ya karoti kuwa vizuri. Mbolea ikizidi sana katika karoti inasabibisha kuwa na  ladha mbaya pia karoti ina kuwa na vimizizi vidogo kama vinyweleo hivyo kupunguza ubora wa karoti.


Kudhibiti Magugu

Palilia shamba mara kwa mara ili kuhakikisha shamba halina magugu. Magugu hudhibitiwa kwa palizi ya jembe, kung’oa kwa mkono ama matumizi ya viuagugu. Matumizi ya viuatilifu yafanyike kila baada ya wiki mbili


Magonjwa Sumbufu ya zao la Karoti

(i) Madoa jani (Leaf Spot)

Ugonjwa huu husababishwa na ukungu na hutokea wakati karoti zina urefu wa sentimita 13 mpaka 15. Hushambulia majani na kuyafanya yawe na madoa yenye rangi nyeusi iliyochanganyika na kijivu au kahawia. Sehemu zinazozunguka madoa haya hubadilika rangi na kuwa njano. Ugonjwa ukizidi majani hukauka.

Zuia ugonjwa huu kwa kunyunyizia dawa za ukungu kama vile Dithane – M 45, Blitox, Copperhydroxide (Kocide), Copper Oxychloride, Cupric Hydroxide (Champion), Antrocol, Topsin M- 70% na Ridomil.

(ii) Magonjwa ya bacteria (bacterial disease).

Huu ugonjwa husababisha kusinyaa kwa mimea (wilting), na kufanya mmea usikue (stunted growth) na shina kuoza (stem rot) pamoja na kuoza kwa karoti.

(iii) Kuoza Mizizi (Sclerotinia Rot)

Ugonjwa huu husababishwa na ukungu na hushambulia mizizi namajani. Dalili zake ni kuoza kwa mizizi na majani. Baadaye sehemu hizi hufunikwa na uyoga mweupe. Kwenye uyoga huu huota siklerotia kubwa zenye rangi nyeusi.

Zuia ugonjwa huu kwa kuzingatiayafuatayo:
a) Epuka kustawisha karoti kwenye maeneo yaliyoshambuliwa na ugonjwa huu.
b) 
Nyunyuzia dawa za ukungu kama vileDithane M- 45, Blitox, Topsin – M 70% na Ridomil.

(iv) Magonjwa ya fangasi (fungal disease) 

kama kata kiuno (damping off) huu ugonjwa hushambulia sana miche hufanya miche ishindwe kukua vizuri na mara nyingi hupelekea mche kufa.


Wadudu Wasumbufu wa Zao la Karoti

i) Minyoo Fundo:

Minyoo hii hushambulia mizizi na kuifanya iwe na vinundu. Hali hii husababisha mmea kudumaa na kupunguza mavuno. Minyoo fundo huweza kuzuiwa kwa kubalidilisha mazao. Baada ya kuvuna usipande mazao ya jamii ya karoti au mazao yanayoshambuliwa na wadudu hawa. Unaweza kupanda mazao ambayo hayashambuliwi na minyoo fundo kama vile mahindi. Pia hakikisha shamba ni safi wakati wote.

ii) Imi wa Karoti

Mashambulizi hufanywa na funza ambaye hutoboa mizizi. Ili kuzuia wadudu hawa tumia dawa kama vile Dichlorvos, Sapa Diazinon na Fenvalerate. Pia badilisha mazao na wakati wa kupalilia pandishia udongo kufunika mizizi.

iii) Karoti Kuwa na Mizizi Mingi (Folking)

Hii hutokea kama karoti zimepandwa kwenye udongo wenye takataka nyingi na usiolainishwa vizuri. Vile vile utumiaji wa mbolea za asili zisizooza vizuri unaweza kusababisba karoti kuwa na mizizi mingi. Hali hii inaweza kuzuiwa kwa kulainisha udongo vizuri na kutumia mbolea za asili zilizooza vizuri.


Jinsi ya Kuvuna Na Kuhifadhi Karoti

Karoti   huvunwa  baada  ya  miezi  mitatu  toka  kupanda  au  kuanzia  wiki  11   hadi  13  kulingana  na  hali  ya  hewa  ya  eneo  ilipolimwa. Karoti  huvunwa  kwa  kung’oa  miche  yake  na  kuchukua mizizi  yake  ambayo  ndiyo  inayotumika  kama  kiungo  katika  vyakula au katika  matumizi  mengine  kama  dawa.

uvunaji wa karoti
Uvunaji wa karoti

Mavuno  ya  karoti  kwa  ekari  moja  ni  kuanzia   tani  10  hadi  15, endapo  utalima  kitaalam (kwa  kutumia  technolojia  za  kilimo  kama   mbegumboleaviuatilifu).

Baada ya  kuvuna  kama  hutauza  hapo hapo hifadhi kwenye baridi ya nyuzi joto moja hadi 4 unaweza hifadhi karoti kwa zaidi ya wiki kabla hujaziuza. Jitahidi upate coldroom hata ya mita tatu kwa tatu ili kujiepushia hasara.


Soko La Karoti

Soko la karoti lipo lina patikana kwa uhakika, kwa sababu karoti inatumika kama kiungo (spice) katika vyakula kama  nyama, wali au  pilau  na vyakula vingine.

Watu wengi hupendelea karoti kutokana na umuhimu wake katika lishe, kwa hiyo soko hupatikana katika mikoa yote Tanzania. Karoti moja inauzwa kuanzia shilingi 100 hadi 200 kulingana na upatikanaji wake eneo  husika. Pia hupimwa kwa kilo kuanzia shilingi 1,000.

Comments

Popular Posts