Wednesday, July 10, 2024

KILIMO BORA CHA BAMIA

 KILIMO BORA CHA BAMIA
Bamia ni zao la mbogamboga linalotambulika kitaalamu kama Abelmoschus esculentus lenye
asili ya Ethipia na Afrika ya magharibi. Kwa sasa zao hili linalimwa katika nchi nyingi hasa
sehemu za joto. Baadhi ya maeneo yanayolima zao la bamia kwa Tanzania ni pamoja na mikoa
ya Morogoro, Dodoma, Tabora, Pwani na Mbeya.
MATUMIZI YA BAMIA
Zao hili hulimwa kwa ajili ya matunda yake ambayo hutumika kama mboga au kiungo katika
mapishi mbalimbali majumbani. Vilevile katika nchi zilizoendelea nyuzi nyuzi zinazotokana na
zao hili hutumika katika utengenezaji wa karatasi.
AINA ZA MBEGU
Kuna aina tofauti za mbegu za bamia zinazo patikana Tanzania kama vile Clemson Spineless,
Emerald Green, White Velvet, Perkins Mammoth na Dwarf Prolific. Mbegu ambazo hutumika
na wengi ni
Clemson spineless. Mbegu hii inatabia ya kukua urefu wa mita 1 hadi 1.5 na kuzaa bamia za
kijani zenye urefu karibu sm 15. Huchukua siku 55 hadi 58 kuanza kuvuna.
Emerald green. Mbegu hii ina tabia ya kukua hadi urefu wa m 1.5 na kuzaa bamia za kijani
zenye urefu wa sm 18 hadi 20. Huchukua siku 58 hadi 60 kuanza kuvuna.
White velvet. Mbegu hii inatabia ya kukua urefu wa m 1.5 hadi 1.8 na kuzaa bamia ndefu,
nyembamba, zilizochongoka na zenye urefu wa sm 15 hadi 18.
Bamia aina ya Emerald green
UCHAGUZI WA ENEO
Ni muhimu kuchagua eneo linalofaa kwa kilimo cha bamia kabla ya kuanza uzalishaji. Ni vyema
eneo litakalotumika katika kilimo cha bamia liwe na urahisi wa upatikanaji maji kurahisisha
umwagiliaji kwa kilimo cha umwagiliaji. Vilevile shamba liwe lenye kufikika kwa urahisi ili
kufanya wepesi katika kuhudumia shamba na usafirishaji wa mazao kwenda sokoni au kufikiwa
kwa urahisi na wanunuzi wanaofuata mazao shambani.
Zao la bamia hushambuliwa sana na minyoo fundo (nematodes). Hivyo usichague eneo ambalo
limetoka kutumika katika kilimo cha mazao yanayoweza kushambuliwa na minyoo fundo kama
vile viazi vitamu, nyanya, bilinganya na pilipili hoho. Kwa tahadhari unaweza kulima zao hili
katika eneo ambalo limetoka kutumika kwa kilimo cha mazao ya nafaka kama vile mahindi na
mtama kwa kuwa mazao haya hayashambuliwi na minyoo fundo.
MAHITAJI YA KIIKOLOJIA
HALI YA HEWA NA MWINUKO
Bamia ni zao linalopendelea hali ya joto hivyo hustawi katika maeneo yenye hali joto kuanzia
nyuzi joto za sentigredi 21 hadi 35. Ustawi mzuri zaidi huonekana katika maeneo yenye joto la
nyuzi za sentigredi 21 mpaka 30. Hali joto zaidi ya nyuzi za sentigredi 42 huweza kusababisha
kudondoka kwa maua. Bamia hustawi vizuri katika maeneo ya mwinuko tofauti hadi mita 1000
kutoka usawa wa bahari yenye mvua za wastani.
UDONGO
Zao la bamia hustawi katika udongo wa aina nyingi wenye rutuba, kina, uwezo wa kuifadhi maji
vizuri na usiotuamisha maji. Hata hivyo zao hili hufanya vizuri zaidi linapolimwa katika udongo
wa tifutifu yenye kichanga wenye rutuba ya kutosha na tindikali kuanzia Ph 5.8 hadi 6.5. Mbegu
za bamia hushindwa kuota kabisa pale joto la udongo linapokuwa chini ya nyuzi za sentigredi
16.
KUANDAA SHAMBA
MUDA WA KUANDAA
Shamba la bamia liandaliwe mapema mwezi mmoja kabla ya kupanda ili kuruhusu magugu na
mabaki ya mazao kuoza vizuri. Kwa kilimo cha kutegemea mvua ni vyema maandalizi yaanze
mapema kabla ya kuanza kwa mvua za masika. Inashauriwa kuanza maandalizi mapema mwezi
Januari. Kwa kilimo cha umwagiliaji unaweza kuanza maandalizi muda wowote kulingana na
mahitaji na soko unalolilenga.
NAMNA YA KUANDAA
Shamba huandaliwa kwa kufyeka nyasi, kung’oa visiki na kulima kabla ya kupima na kuweka
matuta.
(i) KULIMA
Shamba hulimwa kwa kutumia jembe la mkono, jembe la kukokotwa na wanyama, power
tillers au matrekta. Matumizi ya jembe la kukokotwa na wanyama, power tillers na matrekta
hurahisisha shughuli ya kulima na kuifanya iwe na ufanisi kwani hukatua udongo vizuri na
kuufanya uwe tifutifu. Unapotumia jembe la mkono katika kulima hakikisha unakatua udongo
katika kina cha kutosha sm 20 mpaka sm 30 na kulainisha mabonge. Udongo uliokatuliwa vizuri
hupitisha hewa inayohitajika na mmea, hurahisisha ukuaji wa mizizi na kuifadhi maji vizuri.
(ii) KUPIMA SHAMBA (FIELD LAYOUT)
Ni muhimu kuanza kupima shamba kabla ya kuanza kuandaa matuta ili kupata matuta yaliyo
katika mpangilio mzuri na mistari ya mimea shambani iliyonyooka vizuri. Kabla ya kupima
matuta ni muhimu pia kujua nafasi ya kupandia utakayo tumia ili kupata ukubwa sahihi wa kila
tuta.
Kwa mfano kwa nafasi ya kupandia ya sm 60 × sm 40 kwa matuta makubwa unaweza
kutengeneza kila tuta katika upana wa sm 1.2 na urefu wowote. Acha nafasi ya m 1 kuzunguka
shamba na njia kila baada ya tuta upana wa sm 50. Tumia Tape measure au kamba yenye vipimo
kupima shamba huku ukiweka alama za matuta na njia kwa kuchomeka mambo (pegs) katika
kila kona ya tuta na kuzungushia kamba.
(iii) KUWEKA MATUTA
Inashauriwa kupanda bamia katika matuta ili kusaidia mizizi kukua vizuri na udongo kuhifadhi
maji. Wakati wa kiangazi, tengeneza matuta yaliyodidimia kidogo ili kufanya maji yaweze kukaa
kwenye udongo na wakati wa masika matuta yainuliwe kidogo toka kwenye usawa wa ardhi ili
kuzuia maji yasituame. Matuta yanaweza kuwa makubwa au madogo kulingana na matakwa ya
mkulima. Matuta makubwa hupandwa mistari miwili na matuta madogo hupandwa mstari
mmoja. Tengeneza matuta kwa kufuata alama zilizowekwa wakati wa kupima shamba.
UPANDAJI WA BAMIA
Zao la bamia huweza kupandwa moja kwa moja shambani au kwa kuanzia kitaluni. Hata hivyo
wakulima wengi hupendelea zaidi kupanda zao hili moja kwa moja shambani pasipo kupitia
kitaluni. Katika eneo lenye udongo mzito wenye asili ya mfinyanzi mbegu hupata shida kuota
hivyo ni muhimu kuanzia kitaluni ili kuweza kupata miche mingi shambani. Kwa kuanzia
kitaluni hakikisha unafuata taratibu zote za uandaaji na matunzo ya kitalu cha mbogamboga na
pandikiza miche pindi inapokua na majani halisi matatu hadi manne.
MAANDALIZI YA MBEGU
Mbegu za bamia ni ngumu kidogo katika kuota hivyo ni vyema ziandaliwe ili kurahisisha uotaji
wake. Mbegu za bamia huandaliwa kwa kuziloweka katika maji ya vuguvugu kwa muda wa
masaa ishirini na nne ili kuchochea uotaji. Mbegu za bamia huchukua muda wa siku 5 hadi 10
kuota. Kutegemeana na nafasi ya kupandia na uotaji wa mbegu kiasi cha kilo moja na nusu hadi
kilo mbili na nusu za mbegu kinaweza kutosha kupanda katika eneo la ekari moja.
Bamia aina ya clemson spineless
NAFASI YA KUPANDIA
Bamia huweza kupandwa katika nafasi tofauti kuanzia sm 60 hadi 80 kati ya mstari na mstari na
sm 30 hadi 50 kutoka shimo hadi shimo.Hakikisha unafuata maelekezo ya mbegu husika juu ya
nafasi pendekezwa.
HATUA ZA UPANDAJI
Unaweza kufuata hatua zifuatazo katika upanzi wa mbegu za bamia shambani:
1 – Mwagia maji mengi shambani masaa kumi na mbili kabla ya kupanda mbegu ili kulainisha
udongo na kurahisisha upanzi.
2 – Chimba mashimo ya kupandia yenye kina cha sm 2 hadi 3 katika nafasi iliyopendekezwa
kwa mbegu itakayotumika mistari miwili miwili kila tuta kwa kutumia kamba iliyowekwa
vipimo.
3 – Weka viganja viwili vya mkono vya samadi iliyoiva katika shimo la kupandia kisha
changanya na udongo kupata mchanganyiko mzuri. Kwa mbolea ya kupandia kama DAP weka
nusu kizibo cha soda katika kila shimo la kupandia kisha fukia mbolea kwa tabaka dogo la
udongo kabla ya kupanda mbegu. Kiasi cha kilo hamsini za mbolea ya DAP kinatosha kutumika
katika eneo la ekari moja.

No comments:

Post a Comment

Fahamu mbinu za kuongeza thamani nyama

  Safari ya kuongeza thamani nyama ya mifugo huanzia shambani kwa usimamizi wa ufugaji na uzalishaji. Lishe bora ni muhimu kwa wa ufugaji ...