Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Mtandao wa Vikundi vya Wakulima
nchini (MVIWATA) umeiomba Serikali kutunga sheria ndogo ndogo
zitakazowabana wafanyabiashara wa zao la ufuta ili wakulima wapate faida
ya uzalishaji wa zao hilo.
Maombi hayo yamebainishwa hivi
karibuni na Afisa Masoko kutoka MVIWATA, Acquiline Wamba wakati wa
warsha ya uboreshaji wa matumizi ya vipimo sahihi katika biashara ya
mazao ya kilimo iliyofanyika mkoani Dodoma.
Bi. Acquiline amesema Serikali
inatakiwa kuchukua hatua madhubuti kwa kuweka sheria kali dhidi ya
wafanyabiashara wasio waaminifu kwani Sheria hizo zitawasaidia kuwapa
maelekezo ya namna ya kuweka vipimo sahihi kwenye mazao ili kuongeza
ushindani kwenye biashara.
“Wafanyabiashara wasio waaminifu
wamekua ni chanzo cha kukwamisha soko la nje kwa kupeleka mazao yenye
uchafu nje ya nchi, hii sio sahihi ndio maana tunaomba Serikali
itusaidie” alisema Bi. Acquiline.
Aliongeza kuwa ili kuboresha soko
la nje la zao la ufuta Serikali inatakiwa kuhakikisha panakwepo na
mazingira wezeshi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mazao yanayoenda nje ni
masafi.
Aidha, Bi. Acquiline alifafanua
kwamba kuwabana wafanyabiashara wa zao hilo kutumia vipimo sahihi vya
mizani itasaidia kukomesha wafanyabiashara wanaowaibia wazalishaji hao
kwani lengo halisi la kuweka mizani ni kupunguza tabia ya baadhi ya
wafanyabiashara kuongeza mchanga kwenye zao la ufuta kwa lengo la
kuongeza uzito.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Wilaya hiyo, Danford Chisomi alisema kuwa Halmashauri
bado haijawa na mizani ya mazao kutokana na ufinyu wa bajeti hivyo
aliahidi kushiriki katika kutatua changamoto hizo.
“Halmashauri itatafuta nafasi ya
kuweka mizani pamoja na kuunda sheria mpya ndogondogo za kuwadhibiti
wafanyabiashara wa zao hilo”, alisema Chisomi.
Akiongea katika warsha hiyo,
mzalishaji wa ufuta Wilayani Bahi, Fikiri Bernard, alisema kukosekana
kwa mizani katika Halmashauri hiyo kunaathiri moja kwa moja jitihada za
wazalishaji pamoja na kusababisha upotevu wa mapato kwa halmashauri
hiyo.
“Vipimo vingi vinavyotumiwa na
wafanyabiashara huwa haviko sahihi kwa sababu havijahakikiwa na Mamlaka
husika kwa matumizi ya biashara hivyo wafanyabiashara wamekua wakitumia
mwanya huo wa ukosefu wa mizani kuweka vipimo vyao wenyewe vya kununulia
zao la ufuta,” alisema Bernard.
Ameongeza kuwa Halmashauri hiyo
imekua ikipoteza mapato mengi kwa kushindwa kukusanya ushuru kutokana na
kuwepo kwa wafanyabiashara wasio waaminifu wanaopenyeza mazao yao bila
kulipa ushuru.
Vile vile, mkulima huyo ameiomba
Halmashauri kutenga vituo mbalimbali vya kupimia mazao kwa ajili ya
kupata vipimo sahihi vya mazao ili kuepuka kuwaibia wakulima.
No comments:
Post a Comment