Jumatatu, 22 Juni 2026

Jinsi Ruaha Milling inavyowasha mapinduzi ya kilimo cha alizeti na kubadilisha maisha ya wakulima wa Iringa

 

Kwa miaka mingi, kilimo cha alizeti katika maeneo mengi ya Mkoa wa Iringa kilifanyika kwa mazoea. Wakulima walitumia nguvu kubwa mashambani, lakini walivuna kidogo. Waliamini wanafanya kila linalowezekana, lakini mwisho wa msimu walibaki na mavuno yasiyolingana na jasho lao.

Miongoni mwa wakulima hao alikuwa Fausta Kikombe wa Kijiji cha Ikuka, Kata ya Uhambingeto, Wilaya ya Kilolo.

Kwa miaka miwili aliyokuwa akilima alizeti, Fausta hakuwahi kuona matokeo yaliyoweza kumbadilishia maisha. Kutoka katika heka moja na nusu, alikuwa akivuna gunia mbili pekee za alizeti, kiasi ambacho hakikuweza kumwezesha kuongeza kipato cha familia yake wala kufanya uwekezaji wowote wa maana.

“Tulikuwa tunalima kwa mazoea bila kufuata kanuni bora za kilimo. Mavuno yalikuwa madogo sana na wakati mwingine tulilazimika kuuza mazao kwa bei yoyote ili kupata fedha za matumizi ya nyumbani,” anasimulia Fausta.

Simulizi ya Fausta si ya pekee yake.

Ni picha halisi ya maisha ya maelfu ya wakulima wadogo nchini ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya uzalishaji mdogo kutokana na ukosefu wa elimu sahihi ya kilimo, matumizi ya mbegu zisizo bora na kutofikiwa na huduma muhimu za ugani.

Lakini leo, matumaini mapya yanaanza kuonekana katika mashamba ya wakulima wa Ikuka.

Fausta sasa anazungumzia mavuno ya gunia 12 hadi 15 kwa heka moja, kiwango ambacho miaka michache iliyopita kingeonekana kuwa ndoto.

“Kwa elimu tuliyoipata nimeona tofauti kubwa. Sasa ninaamini alizeti inaweza kuwa biashara ya kweli na si zao la ziada kama tulivyokuwa tunafikiri zamani,” anasema.

Tatizo Halikuwa Ardhi, Tatizo Lilikuwa Maarifa

Katika mijadala mingi kuhusu uzalishaji mdogo wa mazao, mara nyingi lawama zimeelekezwa kwenye ukame, mabadiliko ya tabianchi au uhaba wa pembejeo.

Lakini kwa mujibu wa Benjamini Laurence Mbilo, Afisa Shamba Msaidizi wa Ruaha Milling Company Ltd, tatizo kubwa lililokuwa likiathiri wakulima wengi wa alizeti lilikuwa ni ukosefu wa elimu ya uzalishaji wa kisasa.

Mbilo anasema kampuni iligundua hilo baada ya kuona kuwa alizeti nyingi zilizokuwa zikinunuliwa kutoka kwa wakulima zilikuwa na ubora wa chini na kutoa mafuta kidogo wakati wa uchakataji.

“Alizeti nyingi tulizokuwa tunanunua zilikuwa na mapepe mengi na mafuta kidogo. Tulikuwa tunapata mashudu mengi kuliko mafuta. Hapo ndipo tukagundua kuwa suluhisho ni kuwafikia wakulima na kuwapa elimu ya kilimo bora,” anasema Mbilo.

Kauli hiyo ilibadilisha namna kampuni ilivyokuwa ikiangalia biashara yake.

Badala ya kusubiri wakulima walete mazao viwandani, Ruaha Milling iliamua kwenda moja kwa moja mashambani.

Ruaha Milling Yawekeza Kwa Mkulima

Kwa mujibu wa Yasinta Athanasi Kipeto, Meneja wa Masoko wa Ruaha Milling Company Ltd, kampuni hiyo imejenga falsafa yake katika imani kwamba mafanikio ya mkulima ndiyo msingi wa mafanikio ya kampuni.

Anasema Ruaha Milling, ambayo ilianza shughuli zake mwaka 1995 kabla ya kusajiliwa rasmi mwaka 2015, imeendelea kuwekeza katika kuwawezesha wakulima ili kuongeza uzalishaji wa mazao muhimu kama alizeti, mahindi na mpunga.

“Tunategemea mkulima kwa kila hatua ya biashara yetu. Mafanikio ya kampuni hayawezi kutenganishwa na mafanikio ya mkulima, ndiyo maana tunawekeza sana kwenye elimu na uwezeshaji wa wakulima,” anasema Yasinta.

Kupitia mashamba darasa yaliyoanzishwa katika vijiji mbalimbali vya Iringa, wakulima wanafundishwa hatua zote muhimu za uzalishaji kuanzia maandalizi ya shamba, uchaguzi wa mbegu bora, upandaji kwa nafasi sahihi, matumizi ya mbolea hadi uvunaji na uhifadhi wa mazao.

Mbali na mafunzo hayo, kampuni pia imekuwa ikitoa pembejeo kwa mfumo wa mkopo usio na riba huku wakulima wakirejesha gharama baada ya mavuno.

Kilimo Cha Biashara Kinaanza Kueleweka

Moja ya mabadiliko makubwa yanayoonekana kwa wakulima wengi ni kubadilika kwa mtazamo kuhusu kilimo.

Badala ya kukiona kama shughuli ya kujikimu, sasa wanaanza kukiona kama biashara inayoweza kuzalisha faida.

Yasinta anasema kampuni imekuwa ikihamasisha matumizi ya mizani wakati wa mauzo ya mazao ili mkulima ajue kiwango halisi cha uzalishaji wake na mapato anayopata.

“Mkulima anapouza kwa mizani anajua amezalisha kiasi gani na amepata kiasi gani. Hii inamsaidia kufanya kilimo kwa mtazamo wa biashara badala ya mazoea,” anasema.

Anasisitiza kuwa wakulima wengi wenye ardhi kubwa bado wanazalisha chini ya uwezo wao kutokana na ukosefu wa mitaji.

Kwa sababu hiyo, kampuni imekuwa ikiwaunganisha wakulima na taasisi za kifedha ili waweze kupata mikopo ya kuongeza uzalishaji.

Ushirikiano Unaobadilisha Maisha

Katika safari hiyo, Ruaha Milling haiko peke yake.

Kampuni hiyo imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na wadau mbalimbali wa maendeleo, wakiwemo CIAT kupitia mradi wa Tukue kwa Pamoja (Growing Together).

Kwa mujibu wa Inot Ibrahim Songoyani, Bibi Shamba wa CIAT, lengo la mradi huo ni kuwasaidia wakulima kuongeza tija huku wakikabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Tunahamasisha wakulima kupima afya ya udongo, kutumia mbolea za asili kama samadi na kutumia mbegu bora zinazoweza kustahimili mabadiliko ya hali ya hewa,” anasema Inot.

Anasema mashamba darasa yamekuwa darasa halisi kwa wakulima kwani yanawapa nafasi ya kuona tofauti ya matokeo kati ya mbegu bora na mbegu za kawaida.

Mahitaji Makubwa Ya Soko Bado Hayajafikiwa

Licha ya mafanikio yanayoanza kuonekana mashambani, mahitaji ya alizeti kwa ajili ya viwanda bado ni makubwa kuliko kiwango kinachozalishwa kwa sasa.

Yasinta anasema Ruaha Milling inahitaji zaidi ya gunia 15,000 za alizeti kwa mwaka ili kukidhi mahitaji ya uzalishaji.

Anabainisha kuwa kiwanda cha mafuta cha kampuni kina uwezo wa kuchakata kati ya gunia 50 hadi 60 za alizeti kwa siku, huku kila gunia la kilo 70 likitoa wastani wa lita 20 za mafuta.

Hali hiyo inaonyesha kuwa bado kuna fursa kubwa kwa wakulima kuongeza uzalishaji na kunufaika na soko linalokua kwa kasi.

Viongozi Waona Mabadiliko Yakianza

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ikuka, Salum Maginga, anasema elimu inayotolewa kwa wakulima imeanza kuleta mwamko mpya katika jamii.

“Wananchi wetu wanategemea kilimo kwa maisha yao ya kila siku. Kupitia elimu hii wameanza kuona kilimo kwa mtazamo mpya na tunaamini uzalishaji utaongezeka zaidi,” anasema Maginga.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Kijiji cha Ikuka, Zakia Mpogole, anasema kilimo ndicho msingi wa maisha ya wananchi wengi wa eneo hilo.

“Kupitia elimu inayotolewa sasa tunaamini wakulima wataongeza uzalishaji na kipato chao kwa kiwango kikubwa zaidi,” anasema Zakia.


Mbegu Ya Mabadiliko Imeshaota

Kwa Fausta Kikombe, elimu aliyopata imekuwa zaidi ya mafunzo ya kilimo.

Imekuwa mwanzo wa safari mpya ya matumaini.

Kutoka kuvuna gunia mbili katika heka moja na nusu hadi kuwa na matarajio ya kuvuna gunia 12 hadi 15 kwa heka moja, simulizi yake inaonyesha wazi kwamba changamoto kubwa ya mkulima si mara zote ukosefu wa ardhi au mvua.

Wakati mwingine changamoto kubwa ni ukosefu wa maarifa.

Na pale maarifa yanapofika shambani, mavuno huongezeka, kipato huongezeka na maisha huanza kubadilika.

Ndiyo maana kwa wakulima wa Ikuka na maeneo mengine ya Iringa, mapinduzi ya kilimo hayaanzi kwenye viwanda wala kwenye mikutano mikubwa.

Yanaanzia kwa mkulima mmoja anayejifunza mbinu mpya.

Yanaanzia kwenye mbegu moja bora inayopandwa kwa wakati sahihi.

Na yanaanzia kwenye elimu inayoweza kubadilisha maisha ya familia, kijiji na hatimaye taifa zima.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni