Vituo maalum vya kuuzia mazao kuanzishwa

Serikali imepanga kuanza matumizi ya vituo maalum vya kuuzia mazao ili kuwasaidia wakulima kudhibiti ubora wa mazao yao, kupata taarifa za masoko na kuimarisha ushindani wa bei.

Makubaliano ya matumizi ya vituo hivyo yamefikiwa na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Bodi ya Usimamizi Stakabadhi za Ghala na Halmashauri za maeneo yanayotekeleza Mfumo wa stakabadhi.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2017/18, Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema kwamba serikali inahamasisha ushindani kwa kutumia vituo maalum na Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ambao umefanikisha uuzaji wa mazao kwa uwazi na hivyo kumpatia mkulima bei shindani.
“Utaratibu huo umewezesha bei ya Korosho kupanda na kufikia wastani wa Shilingi 3,880 kwa kilo msimu wa 2017/2018 ikilinganishwa na Shilingi 3,346 kwa kilo msimu wa 2016/2017 hivyo mfumo huu ni bora ukilinganisha na utaratibu wa awali” alisema Mwijage.
Aidha, mauzo ya Korosho kupitia Mfumo huo yameongezeka kutoka tani 249,912 msimu wa 2016/2017 hadi tani 291,614 msimu wa 2017/2018 sawa na ongezeko la asilimia 16.7.
Mwijage amevitaja vituo ambavyo vinaendelea kuboresha utendaji wake kuwa ni vya mipaka ya Holili/Taveta, Sirari/Isebania, Namanga/Namanga, Kabanga/Kobero, Rusumo/Rusumo, Mutukula/Mutukula pamoja na Horohoro/Lungalunga.
Aidha, ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Mpakani cha Tunduma/Nakonde upande wa Tanzania ulioanza mwezi Novemba 2016, unatarajiwa kukamilika mwezi Mei 2018. Hadi kufikia mwezi Februari 2018 ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 75.

Comments

Popular Posts