Wednesday, June 17, 2026

TANZANIA KUNUFAIKA NA UWEKEZAJI MPYA WA PARACHICHI NA CHAI: WAZIRI CHONGOLO AIPOKEA KAMPUNI YA FRONTIER



Serikali imeendelea kuimarisha jitihada za kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Kilimo baada ya Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), kukutana na ujumbe wa wawekezaji kutoka Kampuni ya Frontier ulioongozwa na Mtendaji Mkuu wake, Bw. Lars Tushuizen, jijini Dodoma.

Mazungumzo hayo yalijikita katika fursa za uwekezaji kwenye mazao ya kimkakati ya Parachichi na Chai, huku pande zote zikikubaliana kuhusu umuhimu wa kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani ya mazao hayo na kupanua masoko ya ndani na nje ya nchi kwa manufaa ya wakulima na uchumi wa Taifa.

Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Lars Tushuizen alisema Kampuni ya Frontier ina nia ya kuwekeza katika maendeleo ya mnyororo wa thamani wa mazao ya Parachichi na Chai kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa zinazolenga kuongeza tija katika uzalishaji, uchakataji na usambazaji wa mazao hayo.

Alieleza kuwa Tanzania imeendelea kuwa kivutio kikubwa kwa wawekezaji kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji pamoja na uwezo mkubwa wa uzalishaji wa mazao hayo, hali inayoweza kuchangia ongezeko la mapato kwa wakulima na kukuza uchumi wa nchi.

“Tanzania ina fursa kubwa katika uzalishaji wa Parachichi na Chai. Kupitia uwekezaji wa teknolojia za kisasa, tunaamini tunaweza kusaidia kuongeza thamani ya mazao haya na kufungua masoko mapya yenye tija kwa wakulima,” alisema Bw. Tushuizen.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo, aliukaribisha uwekezaji huo na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wote wenye dhamira ya kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini.


Alisema Wizara ya Kilimo imejipanga kuendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha uwekezaji, kuongeza ushindani wa mazao ya Tanzania katika masoko ya kimataifa na kuhakikisha wakulima wananufaika zaidi kupitia ongezeko la thamani na upatikanaji wa masoko yenye uhakika.

“Serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji wanaokuja kuongeza thamani katika Sekta ya Kilimo kwa lengo la kuongeza tija, ajira na mapato kwa wananchi pamoja na Taifa kwa ujumla,” alisisitiza Mhe. Chongolo.

Uwekezaji unaolengwa katika mazao ya Parachichi na Chai unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya sekta hiyo, hasa katika maeneo ya uzalishaji, usindikaji, uhifadhi na upanuzi wa masoko ya kimataifa, jambo ambalo linaweza kuongeza ushindani wa mazao ya Tanzania katika soko la dunia.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Mha. Athumani Kilundumya; Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Prof. Peter L. M. Msoffe; Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania, Bi. Beatrice Banzi, pamoja na maafisa waandamizi wa Wizara ya Kilimo.



Hatua ya Kampuni ya Frontier kuonesha nia ya kuwekeza katika mazao ya Parachichi na Chai ni ishara ya kuendelea kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji nchini. Ikiwa uwekezaji huo utatekelezwa kwa mafanikio, unaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza thamani ya mazao, kuboresha kipato cha wakulima na kuimarisha mchango wa Sekta ya Kilimo katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

No comments:

Post a Comment