Mambo matano ya muhimu kuyafahamu kabla ya kuwekeza kwenye Kilimo
Leo hii napenda
tuanze kujifunze mambo matano ambayo kila mtu aliye na ndoto ya
kuwekeza kwenye kilimo ni lazima ayafahamu vizuri. Kutotilia maanani
moja ya mambo haya kunaweza kupelekea ukakichukia kilimo. Leo tutaanza
na mambo mawili.
1 Soko
Hili ndilo jambo la
muhimu kwenye kila uwekezaji au kwa maana nyingine biashara yeyote
lazima itegemee soko.Na hapa ndipo wengi wanakosea sana wakulima
wadogo na hata vijana wanaoingia kwenye kilimo maana wengi wanazalisha
kwa kufuata mkumbo kwa vile wengi wanazalisha wakati huo au amesikia
labda kilimo cha zao Fulani kinalipa. Kabla ya kuwekeza kwenye kilimo
lazma uanze kwa kulitambua soko lako.
Lazima uzalishaji wako uwe
unaendeshwa na soko. Unatakiwa kua na taarifa za kutosha kuhusu soko,
kujua soko linasemaje, ni wakati gani watu wengi wanakua wamezalisha,
wakati gani bidhaa hii inakua kwa wingi sokoni, ni wakati gani inakua
hadimu na ni kwanini? Usizalishe kwa vile ni msimu wa kuzalisha kwamba
unaona mko wengi. Watu wengi wanaofaidika kwenye kilimo ni wale ambao
hawafuati mkumbo kwenye kuzalisha wao wanajua kucheza na wakati, wakati
bidhaa ile ni hadimu au wakati ambao sio msimu wa kuzalisha, ndio wakati
wa wao kuzalisha na hivyo kupelekea kupata faida nzuri zaidi. Hata
kampuni kubwa zinazowekeza kwenye kilimo kwanza wanakua na soko la
uhakika, aidha baada ya kufanya utafiti wa kutosha au kwa kuingia
mikataba na wateja wao. Vyovyote vile lakini wanchokua na uhakika nacho
ni kua wanajua ni wapi watauza baada ya kuzalisha. Mfano kwa kampuni
zinazozalisha maua Arusha na maeneo mengine soko lao kubwa liko uholanzi
(Amsterdam Auction) na ndio maana asilimia kubwa ya wamiliki wa kampuni
hizo ni waholanzi maana wanalijua vizuri soko la maua. Ila kwetu hali
ni tofauti badala ya kuanzia sokoni sisi tunaenda moja kwa moja shambani
kuzalisha baada ya mazao kukomaa na kua tayari kuvuna ndio
tunalikumbuka soko, yaan umeshazalisha ndo unaenda kutafuta soko, bila
kujua pengine ulichonacho hakihitajiki na soko.
Wengine wanaweza
kusema hatuwezi kuwekeza kwenye kilimo maana soko hakuna, hasa wakulima
wadogo wengi wanafahamu soko ni pale kwenye mkusanyiko wa watu wengi
kama kwenye minada, magulio au kwenye masoko kama kilombero arusha,
mabibo dar n.k. Unachotakiwa kujua ni kwamba kuna aina kadhaa za
masoko mfano masoko ya ndani yasiyo rasmi, masoko ya kitaasisi  kama
mahoteli, mashule na mahospitali. Pia kuna masoko ya kiviwanda; Â mfano
viwanda vya kuongeza thamani kama vya azam au Redgold arusha n.k Bila
kusahau masoko ya kimataifa kama ulaya, asia na hata nchi za jirani kama
Sudan ambako kumekua na vita na watu wamekua hawana muda wa kuzalisha.
Hata hivyo kuna vitu vingi sana vya kujifunza kwenye upande wa soko
naona kwa leo tuishie hapa kwa upande wa soko, tukipata muda huko
mbeleni tutajadili kwa kina.
2 Hali ya hewa inayoruhusu kilimo husika
Kila kilimo cha zao
fulani kina hali ya hewa au mazingira yanayo kiruhusu kilimo hicho
kustawi vizuri.
Kwenye eneo hili tunaangalia maswala ya jotoridi,
unyevunyevu kwenye hewa, mvua na sifa za udongo unaosaidia ukuaji wa zao
husika. Kuna mazao yanapendelea hali ya joto na kuna mengine yanastawi
kwenye hali ya baridi. Mfano kama mananasi yanapendelea ukanda wa joto
na ndio maana yana stawi sana ukanda wa pwani huko. Katika sifa za
udongo kuna sifa za kikemikali au kifikzikia. Mfano wa sifa hizo ni kama
pH ambacho ni kipimo cha kiwango cha asidi na alikali ya udongo. Hii
ina maana pH ya udongo wako ikiwa ndogo chini ya 5 udongo wako una
kiwango cha asidi na ikiwa kubwa zaidi ya 8 maana yake udongo wako una
kiwango fulani cha alikali. Katika aina ya udongo inakubidi ufahamu ni
udongo mfinyanzi, tifutifu au kichanga. Usije ukapanda mpunga kwenye
udongo wa kichanga wakati mpunga unapendelea udongo unaotuamisha maji.
Au unapanda vitungu kwenye udongo unashikamana sana (mfinyanzi) wakati
kitunguu kinahitaji udongo wenye kuachia (tifutifu) ili kiweze kujijenga
vizuri. Lakin ngoja nisiingie kwa kina sana hapa kwenye udongo maana
kuna mambo mengi sana na ndio maana watu wanasomea shahada za chuo kikuu
kwenye masuala ya udongo na hata wengine wanakua maprofesa wa udongo.
Lengo la kukupitisha
hapa kidogo ni ili ufahamu kwamba baada ya kupata soko la uhakika na
kujua ni zao gani kinachofuata ni kujua maeneo gani zao hilo linastawi,
ni udongo wa aina gani unaofaa. Unashauriwa kabla ya kupanda uchukue
sampuli ya udongo ukapime maabara kujua sifa za udongo wa shamba lako.
Zipo taasisi za serikali na binafsi zinazotoa huduma ya upimaji udongo.
Taasisi hizo ni kama taasisi za utafiti wa kilimo kama SARI (Arusha) ARI
Ukiliguru ( Mwanza), ZARI Kizimbani (Zanzibar), ARI Maruku Kagera, ARI
Kibaha n.k Pia zipo taasisi za elimu kama Chuo Kikuu cha Kilimo cha
Sokoine (SUA) Mororgoro. Ukishapima udongo unapewa ushauri wa zao gani
linaweza kustawi vizuri kwenye shamba lako lakini pia unapata ushauri wa
aina gani ya mbolea unatakiwa kutumia. Gharama ya upimaji inategemea na
wingi wa vitu unavyotaka kupima kwenye huo udongo.
Kwa kifupi maeneo
mengi ya nchi yetu ni mazuri sana kwa kilimo na ndio maana tunaona nchi
nyingi zinakuja kuwekeza kwenye kilimo nchini kwetu. Hata hapa kwenye
jumuiya ya afrika mashariki wenzetu wanaimezea mate sana ardhi yetu
yenye rutuba. Nchi ya Tanzania inauwezo mara kumi ya Kenya au kwa maneno
mengine ina hali ya hewa nzuri katika kuzalisha mbogamboga mara kumi
zaidi ya Kenya, maeneo mengi ya Kenya ni makame sana. Lakin cha
kushangaza wenzetu wanazalisha mazao hayo na kuuza nje ya nchi mara kumi
zaidi ya Tanzania. Je ni kwanini? Basi naomba tukutane tena wiki
ijayo hapa hapaKwa ushauri au maswali waweza wasiliana na Ndugu Deogratias macha
amabaye ni mwandishi mwandamizi wa maswala ya kilimo , mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo.
Unaweza kuwasiliana nae kwa simu 0756 483 174 au email deogratiasmacha@gmail.com au tupashanehabari@gmail.com
Comments
Post a Comment