Saturday, May 12, 2018

Mwongozo wa Kilimo Bora cha Papai



Utangulizi:
Mapapai ni zao moja kati ya mazao ya matunda yenye vitamini A na madini ya kalsiamu kwa
wingi. Inaamanika asili ya papai, ni huko nchi za Amerka ya kati, (Mexico), ndipo zao ili likasambaa duniani kote. Kwa sasa zao hili hulimwa karibu kila mahali hapa nchini. Papai ni moja ya mazao yenye faida kubwa na yenye soko la uhakika. Ekari moja ya papai ikitunzwa vizuri inaweza kukupatia faida ya zaidi ya milioni 20 kwa kipindi cha miaka 2 hadi 3.
Kuna aina 3 za mbegu za papai.

1. Mbegu za kienyeji (local varieties). hizi ni aina ya papai za kienyeji ambazo, mara nyingi hazifahamiki majina yake. Mbegu zake huwezi zipata kwenye mfumo rasmi wa mbegu (madukani) nk. mara nyingi mbegu hizi hupatikana kwa kuchukua matunda yaliyoiva na kuchukua mbegu zake.. kiswahili cha mtaani husema mbegu za kukamua..
2. Aina za kawaida (open pollinated varieties kwa kifupi OPV). Mfano wake ni kama Calina nk hizi hua na uzao wa kati.
3. Chotara (hybrid). Mfano Malkia F1, Sinta F1, Red royal mk. Hizi hufanya vizuri maeneo mengi.. hua na uzao mkubwa kuliko aina nyingine tulizojifunza hapo juu
MAMBO YA KUZINGATIA WAK ATI WA UZALISHAJI
Ili kupata mazao yenye ubora unaotakiwa ni muhimu kuzingatia kanuni za kilimo bora za uzalishaji
wa mapapai. Ubora wa matunda baada ya kuvunwa hutegemea jinsi yalivyozalishwa. Baadhi
ya kanuni hizo ni kama zifuatazo:
Kuchagua aina bora
Chagua aina bora ya kupanda kulingana na mahitaji ya soko.
Kudhibiti wadudu, magonjwa na magugu
Mapapi hushambuliwa kwa urahisi na magonjwa na wadudu, hivyo ni muhimu kufanya ukaguzi
wa mara kwa mara ili kugundua dalili za mashambulizi.
Endapo kuna dalili za mashambulizi, dhibiti mapema ili kuzalisha mazao bora yanayoweza
kuhifadhiwa kwa muda mrefu.
Pia hakikisha shamba na barabara zake ni safi wakati wote ili kurahisisha uvunaji na
usafirishaji.
Maandalizi kabla ya kuvuna
Kukagua shamba
Kagua shamba kuona kama kuna mapapai yaliyokomaa
Mapapai hukomaa katika kipindi cha miezi minne hadi mitano kutoka maua yanapochanua.
Dalili za mapapai yaliyokomaa
Tunda hubadilika rangi kutoka kijani kibichi na kuwa ya kijani nyepesi hadi manjano.
Kuandaa vifaa vya kuvunia, kufungashia na kusafirishia
Vifaa vya kuvunia
Vichumio
Mifuko
Ngazi
Vifaa vya kufungashia
Makasha ya mbao/ plasitiki au makaratasi magumu
Vyombo vya kusafirishia
Mikokoteni
Magari
Matela ya matrekta
Kuvuna
Uvunaji bora wa mapapai ni wa kutumia mikono ambapo tunda huchumwa kwa mkono au kwa kutumia vichumio maalumu.
Vuna mapapai yaliyokomaa tu
Vuna mapapai pamoja na vikonyo vyake
Vuna kwa uangalifu ili kuepuka kudondosha matunda
Matunda yakidondoka, huchubuka, hupasuka au hupondeka hivyo husababisha upotevu.
W eka mapapai kivulini mara baada ya kuvuna
Kuchambua, Kusafisha na Kupanga Madaraja
Ni muhimu kuchambua mapapai ili kutenga yaliyooza, kupasuka na yenye dalili za magonjwa au kubonyea. Lengo la kuchambua ni kupata matunda yenye ubora kulingana na matumizi , kwa mfano kusindika, kuuza au kusafirisha.
Matunda yaliyooza na yenye wadudu ni vyema yafukiwe ili kuangamiza wadudu waharibifu
na vimelea vya magonjwa, na pia kuzuia kuenea kwa wadudu na magonjwa hayo.
Matunda yaliyopasuka, kubonyea au kuchubuka kidogo yatumike haraka kwa kuliwa.
Matunda mazuri ambayo hayajapata madhara yoyote yatumike kwa ajili ya kusindika, kuliwa, kuuzwa au kusafirishwa.
Kilimo cha Viazi Vitamu (sweet Potatoes)

Kilimo cha Viazi Vitamu (sweet Potatoes)


Viazi vitamu ni moja kati ya mazao makuu ya mizizi nchini Tanzania ambalo hulimwa kwa ajili ya chakula. Zao hili ni moja kati ya mazao ya kinga ya njaa kutokana na sifa yake ya kuvumilia ukame. Zao la viazi vitamu, asilia yake ni Amerika ya Kati na ya Kusini. Nchini Tanzania, zao hili hulimwa zaidi katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Dodoma, Morogoro, Kagera, Arusha na Ruvuma.
Matumizi
Viazi vitamu hutumika kama chakula kwa kutayarishwa katika njia mbalimbali kama vichembe, na Matobolwa. Pia Unga wa viazi vitamu hutumika kutengeneza vyakula kama keki, maandazi, kalimati, tambi na Juice. Majani ya viazi huliwa kama mboga pia hutumika katika kutayarisha mboji.

Aina
Kuna aina nyingi za viazi vitamu zinazolimwa ulimwenguni. Hapa nchini Tanzania aina zinazolimwa zaidi ni Ukerewe, Simama, Kakamega, Karoti C, Mwananjemu, Ali mtumwa mayai, Mavuno, Pananzala, Kibakuli, Sinia,Vumilia, Kabode, na Polista
Uzalishaji
Zao hili hustawi maeneo mengi Nchini Tanzania. Viazi hustawi vizuri katika maeneo ya tambarare yenye udongo tifutifu, unaoruhusu maji kupenya kwa urahisi. Udongo wa mfinyazi na wenye kokoto nyingi haufai kwani huzuia mizizi kupenya na kupanuka.
Shamba jipya litayarishwe vizuri kwa kufyeka vichaka na kungoa visiki. Majani yafukiwe wakati wa kutengeneza matuta ili kuongeza rutuba ya udongo.
Viazi vipandwe kwa kutumia Marando yenye urefu wa sentimita 30 kwa mavuno bora. Inashauriwa kutumia sehemu ya juu ya shina kwa mavuno zaidi. Marando yapandwe katika umbali wa sentimita 25 hadi 30 kutoka mmea hadi mmea na sentimita 60 hadi 75 kutoka tuta hadi tuta. Viazi pia vyaweza kupandwa kwa kutumia viazi vyenye afya vyenye uzito wa kati ya gramu 20 hadi 30. Hata hivyo inashauriwa kutumia marando ili kupata mavuno zaidi na kuepuka kuenea kwa magonjwa.
Kutunza shamba
Ni muhimu kupalilia viazi vitamu katika miezi miwili ya mwanzo ili kuupa mmea nguvu ya kutambaa vizuri. Baada ya muda huo, viazi huweza kufunika ardhi na hivyo huzuia uotaji wa magugu.
Viazi hushambuliwa na wadudu mbalimbali wakiwemo kipepeo, mbawa kavu, fukusi na minyoo fundo.Pia hushambuliwa na magonjwa yakiwemo magonjwa yanayotokana na virusi kama Sweet Potato Chlorotic Stunt virus (SPCSV). Magonjwa na wadudu yaweza kudhibitiwa kwa kuzingatia usafi wa shamba, kubadilisha mazao, na kuzingatia udhibiti sango.
Uvunaji
Viazi vitamu huwa tayari kuvunwa miezi mitatu hadi minne tangu kupanda kutegemea hali ya hewa. Viazi vinaweza kuvunwa kidogo kidogo kwa kutumia mikono, vijiti, jembe, au rato kadri vinavyohitajika. Aidha inashauriwa viazi visiachwe ardhini muda mrefu bila kuvunwa kwani vitakomaa sana na kuwa na nyuzi, na hivyo kuharibu ubora wake. Pia kuacha viazi muda mrefu hukaribisha mashambulizi ya wadudu kama fukusi na kuoza. Kwa maeneo makubwa zaidi, inashauriwa kutumia mashine ya kukokotwa na ngombe. Uvunaji ufanywe kwa uangalifu ili kuhakikisha viazi visikatwekatwe wala kuchubuliwa wakati wa kuvuna.
Mavuno ya viazi hutofautiana kulingana na aina, hali ya hewa, na udongo. Mavuno ya viazi yanakadiriwa kufikia tani 20 kwa hekta.
Kwa mahitaji ya mbegu za viazi vitamu au ushauri wowote kuhusu kilimo wasiliana nasi kupitia:
simu; 0756 483 174
Email:tupashanehabari@gmail.com

Faida za Miparachichi, Miembe na Michungwa

Faida za Miparachichi, Miembe na Michungwa

  • Miparachichi imekuwepo nchini kwa miaka mingi. Katika mikoa ya kaskazini (Kilimanjaro na Arusha) pamoja na kutumika kama matunda, maparachichi yalibeba jina la chakula cha mbwa kwa kuwa mara nyingi yalipodondoka kutoka kwenye miti yaliliwa na mbwa. Hata hivyo, mikoa ya kusini (Mbeya) maparachichi yamekuwa tunda muhimu katika milo yote.

  • Utafiti umeonesha kwamba maparachichi yana mafuta muhimu yanayoondoa mafuta yanayoganda kwenye mishipa ya damu. Pia yana virutubisho vinavyofanya damu itembee kwa urahisi mwilini. Maparachichi yana virutubisho vya vitamini E. Kwa sababu hii maparachichiyanatumika katika kutengeneza vipodozi ya ngozi na nywele.
  • Matunda ya parachichi yanaweza kuliwa kwa namna tofauti. Yanaweza kuliwa kama kituliza njaa wakati ukisubiri chakula kingine au kilainisha chakula baada ya mlo. Pia parachichi linaweza kuliwa sambamba na chakula kingine kwa mfano ndizi za kuchoma. Maparachichi yanatumika pia kutengeneza juisi.
  • Matunda machanga yaliyoanguka yanatumika kuharakisha uivishaji wa ndizi kwa kuzifanya ndizi ziive zote kwa pamoja.
  • Majani ya miparachichi yanatumika kulishia mifugo kama mbuzi na ngombe wakati miti yake inatoa mbao nzuri za kutengenezea samani.
  • Hivyo miparachichi inaweza kuwa chanzo kizuri cha pesa kwa familia na wajasiliamali soko lake likiboreshwa.
  • Miparachichi huweza kustawi sehemu nyingi zenye hali ya hewa ya kitropiki iliyo na kipindi cha ubaridi, joto kiasi na mvua za kutosha.
  • Hivyo, hapa nchini kilimo chake kimeshamiri zaidi kwenye maeneo ya nyanda za juu mikoa ya Mbeya, Iringa, Morogoro, Kilimajaro na Arusha. Sehemu nyingine zilizo kwenye miinuko mfano Lushoto mkoani
  • Tanga zao hili laweza kulimwa. Hata hivyo kulingana na aina ya miparachichi, maeneo ya nyanda za chini yasiyo na vipindi virefu vya ukame yanaweza pia kustawisha zao hili. Kwa vile miparachi ni miti inayo kua haraka na haipukutishi majani, hivyo ni mti mzuri katika kuhifadhi mazingira.
  • Endapo miti hii itapandwa kwa wingi itakuwa ni kivuto cha ukusanyaji wa hewa ya ukaa inayotokana na ongezeko la mabadiliko ya tabia nchi.
1.2 MIEMBE
  • Embe ni tunda maarufu na limekuwa likitambulika kama mfalme wa matunda. Matunda ya embe yanatumika yakiwa mabichi au yameiva. Matunda yaliyoiva yanaliwa kama tunda au pia yanaweza kutengenezwa juisi na jam.
  • Embe mbichi hutumika katika kutengeneza achali. Kama ilivyo kwa miparachichi, miembe hukua haraka na haipukutishi majani na hivyo ni mti unaobadilisha mazingira ya mashamba na kuleta hali ya ukijani kwa mwaka mzima.
  • Miti ya miembe ikipandwa kwa mpango mzuri mashambani inasaidia kurekebisha hali ya hewa kwa kupunguza joto, kuvuta mawingu ya mvua, kupunguza kasi ya upepo, kupunguza mmomonyoko wa ardhi na kufyonza hewa ya ukaa.
  • Hivyo Miembe nayo ni miti mizuri kwa kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
  • Miti hii ikipandwa mashambani kwa mpangilio mzuri wakulima wataweza kulima mazao menginena hivyo kujipatia fedha zaidi, matunda na hata kuni.
  • Miembe hustawi sehemu zenye joto la wastani na lenye maji au mvua za kutosha, hata hivyo miembe haistawi vizuri katika maeneo yenye baridi kali na mvua nyingi kwa mwaka kwa kuwa inahitaji kipindi cha ukame cha miezi isiyopungua miwili hadi mitatu ili kuwezesha kutoa maua. Pia miembe hihutaji udongo wenye kina usio twamisha maji na usio na chumvi chumvi.
1.3 MICHUNGWA
  • Michungwa pamoja na aina ya matunda yaliyo kwenye jamii yake kama vile machenza, madaransi, mapomelo, malimau, ndimu n.k. pia ni matunda maarufu katika sehemu za nchi za joto na zile za joto kiasi.
  • Matunda haya hutumika mara nyingi yakiwa yameiva kwa kuyala moja kwa moja au kutengeneza juisi na jam.
  • Yana vitamini C nyingi pamoja virutubisho vingine vinavyohitajika kwa mwanadamu.
  • Machungwa pamoja na jamii yake huwapa wakulima faida wakati wa mauzo na pia huongeza thamani ya mashamba yao. Wadau wengi hunufaika kutokana na kilimo cha matunda haya. Kwa mfano walanguzi na wafanya biashara wengine kama wale wasafirishaji hujipatia faida.
  • Miti ya michungwa kama ilivyo kwa miti mingine, kutumia hewa ya ukaa na hutengeneza kivuli na hivyo kupoza joto.
  • Michungwa huweza kustawi kutoka ukanda wa pwani hadi sehemu za miinuko ya kiasi cha mita 2000 kutoka usawa wa bahari. Pia miembe hihutaji udongo wenye kina usio twamisha maji na usio na chumvi chumvi.
  • Machungwa pia huhitaji kipindi kifupi cha ukame ambapo baada ya kupata maji hutoa maua.

Vituo maalum vya kuuzia mazao kuanzishwa

Serikali imepanga kuanza matumizi ya vituo maalum vya kuuzia mazao ili kuwasaidia wakulima kudhibiti ubora wa mazao yao, kupata taarifa za masoko na kuimarisha ushindani wa bei.

Makubaliano ya matumizi ya vituo hivyo yamefikiwa na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Bodi ya Usimamizi Stakabadhi za Ghala na Halmashauri za maeneo yanayotekeleza Mfumo wa stakabadhi.
Akizungumza wakati wa kuwasilisha bajeti ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2017/18, Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema kwamba serikali inahamasisha ushindani kwa kutumia vituo maalum na Mfumo wa Stakabadhi za Ghala ambao umefanikisha uuzaji wa mazao kwa uwazi na hivyo kumpatia mkulima bei shindani.
“Utaratibu huo umewezesha bei ya Korosho kupanda na kufikia wastani wa Shilingi 3,880 kwa kilo msimu wa 2017/2018 ikilinganishwa na Shilingi 3,346 kwa kilo msimu wa 2016/2017 hivyo mfumo huu ni bora ukilinganisha na utaratibu wa awali” alisema Mwijage.
Aidha, mauzo ya Korosho kupitia Mfumo huo yameongezeka kutoka tani 249,912 msimu wa 2016/2017 hadi tani 291,614 msimu wa 2017/2018 sawa na ongezeko la asilimia 16.7.
Mwijage amevitaja vituo ambavyo vinaendelea kuboresha utendaji wake kuwa ni vya mipaka ya Holili/Taveta, Sirari/Isebania, Namanga/Namanga, Kabanga/Kobero, Rusumo/Rusumo, Mutukula/Mutukula pamoja na Horohoro/Lungalunga.
Aidha, ujenzi wa Kituo cha Pamoja cha Mpakani cha Tunduma/Nakonde upande wa Tanzania ulioanza mwezi Novemba 2016, unatarajiwa kukamilika mwezi Mei 2018. Hadi kufikia mwezi Februari 2018 ujenzi wa kituo hicho umefikia asilimia 75.
Washindi wa shindano la ubunifu wa kiteknolojia katika picha ya pamoja na mgeni rasmi baada ya kukabidhiwa zawadi zao

**
Wataalamu mbalimbali walioudhuria kongamano la The East Africa (EA) Innovation Event la kampuni mama ya TBL Group ya ABInBev lenye lengo la kuleta mapinduzi ya kilimo kupitia sayansi na teknolojia lililoandaliwa na taasisi ya Bits&Bites Technology Convention na kufanyika jijini Dar es Salaam, wamedhihirisha kuwa mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo nchini na barani Afrika kwa ujumla yanawezekana kupitia matumizi ya teknolojia za kisayansi.

Kongamano hilo ambalo lilijumuisha wataalamu wa fani ya kilimo,watafiti,wahandisi na wabunifu kutoka kanda ya Afrika Mashariki walijadili jinsi ya kupata ufumbuzi wa kuinua kilimo cha wakulima wadogo kupitia teknolojia za kisasa na za gharama nafuu ambapo pia walishiriki shindano la ubunifu wa nyenzo za kiteknolojia ambapo walipata fursa ya kuwasilisha kazi zao walizogundua.

Makampuni ya Imara Tech,Mobisol na Back Save Equipment yaliibuka na ushindi baada ya jopo la majaji waliokuwa wanasimamia shindano hilo kubainisha kuwa ugunduzi wao wa nyenzo za kiteknolojia unaweza kusaidia kuinua maisha ya wakulima wadogo.Kazi zilizowapatia ushindi washiriki zitaanza kufanyiwa majaribio kabla ya mchakato wa kuzifikisha kwa walengwa ambao ni wakulima hususani wadogo wadogo.


Akiongea wakati wa kufunga kongamano hilo, Mkurugenzi wa taasisi ya Tanzania Private Sector Foundation (TPSF), Godfrey Sembeye, alisema kuwa kongamano hili limefanyika kwa wakati mwafaka ambapo Tanzania inajipanga kuingia katika uchumi wa viwanda ambao unaenda sambamba na kufanya mapinduzi ya kilimo kwa ajili ya kupata malighafi ya viwanda vitakavyoanzishwa,pia kuwa na uhakika wa chakula cha kutosha.

Sembeye, alisema njia pekee ya kuleta mapinduzi ya kilimo ni kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa na za gharama nafuu ambazo wakulima wengi wa hali ya chini wanaweza kumudu kuzinunua na kuzitumia kwa ajili ya kuwawezesha kupata tija na ufanisi katika kazi zao.


“Kutokana na taarifa za tafiti mbalimbali imebainishwa kuwa bara la Africa lina hekari 600 milioni ambazo hazitumiki ambazo zikitumika ipasavyo zitaweza kuzalisha chakula cha kulisha watu wapatao bilioni 9 hadi kufikia mwaka 2050 na ardhi hii haitanufaisha bara la Afrika tu bali dunia nzima, sekta ya kilimo inaonekana kuwa na fursa kubwa, kinachotakiwa ni kujipanga kuhakikisha inaenda sambamba na mabadiliko ya kiteknolia yanayobadilika kila siku”,alisema Sembeye.

Sembeye aliipongeza kampuni ya TBL Group na ABInBev kwa kuanzisha mkakati wa kushirikiana na makampuni ya wasomi wabunifu kutafuta njia ya kuwawezesha wakulima wadogowadogo kuongeza uzalishaji kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa “Nawaasa mhakikikishe kazi za washindi wa leo na mawazo mazuri yaliyopatikana kwenye kongamano hilo yafanyiwe kazi kwa lengo lililokusudiwa la kuongeza uzalishaji kwa wakulima wadogo kupitia teknolojia za kisasa.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Mpango wa Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGGOT), Geoffrey Kirenga ,alisema kuwa wakati umefika sasa wa watanzania kuchangamkia fursa zilizopo kwenye kilimo badala ya kubaki nyuma kama watazamaji.

Aliwataka pia wasomi wa kitanzania kuendelea kufanya tafiti mbalimbali za kuboresha sekta ya kilimo sambamba na ubunifu wa nyenzo za kisasa na kuongeza kuwa vijana ambao ni wengi wasiogope kujiingiza huko kwa kuwa kuna fursa kubwa “Tunapoongelea kilimo cha kisasa na cha kisayansi hatupaswi kuwaacha vijana nyuma kwa kuwa ndio watumiaji wakubwa wa vifaa vya teknolojia za kisasa,wakivitumia kwa shughuli za kilimo wanaweza kunufaika na kuinua maisha yao”, alisema.


Mkurugenzi wa kitengo cha sheria na Masuala ya Ndani wa kiwanda cha bia cha Nile,nchini Uganda kilichopo chini ya kampuni ya ABINBEV,Onapito Okomoloit,, alisema katika ukanda wa Afrika Mashariki wapo maelfu ya wakulima wadogowadogo wa zao la Shahiri na mtama wanaoshirikiana na kampuni ya ABInBev katika nchi za Tanzania na Uganda kupitia kampuni zake tanzu za Tanzania Breweries Limited (TBL) na Nile Breweries Limited (NBL),ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa mvua,wakiwezeshwa kiteknolojia wataongeza uzalishaji na maisha yao kuwa bora.

Mwanzilishi wa taasisi ya Bits&Bytes Convention,Zuweina Farah ,amesema kuwa kongamano la mwaka huu limepata mafanikio makubwa hususani kwa kutoka na maazimio ya kupambana na changamoto za wakulima wadogo na kuzitafutia ufumbuzi lengo kubwa likiwa ni kuwakwamua.

Saturday, May 5, 2018

Serikali yawahakikishia mbolea kuwafikia wakulima

Serikali itahakikisha kuwa mbolea inawafikia wakulima kwa wakati katika msimu ujao ili kuchochea ukuaji wa sekta ya kilimo hapa nchini hali itakayoongeza ari ya utekelezaji wa dhana ya ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Akizungumza Bungeni mjini Dodoma Waziri wa Kilimo Mhe. Dkt. Charles Tizeba amesema kuwa katika msimu ujao, Serikali imejipanga kuhakikisha kuwa wakulima wanapata mbolea na pembejeo nyingine katika maeneo yao wakati wote wanapohitaji.
“Tutaandaa utaratibu maalum wa kuwajengea uwezo wabunge wote kuhusu utaratibu mpya wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja ili Waheshimiwa Wabunge waweze kutoa maoni yao hali itakayosaidia kuboresha mfumo tuliouweka wa uagizaji wa mbolea kwa pamoja”, alisisitiza Dkt. Tizeba
Akifafanua zaidi, Dkt. Tizeba amesema kuwa ni matumaini yake kuwa baada ya wabunge kujengewa uwezo watakuwa na uelewa mzuri kuhusu utaratibu huo hali itakayoondoa sintofahamu iliyopo kuhusu utaratibu mpya wa uagizaji na usambazji wa mbolea kwa pamoja.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Dkt. Mary Mwanjelwa, akijibu swali la mbunge wa Hanang Dkt. Mery Nagu aliyetaka kujua ni kwa nini vocha zimepungua na lini Serikali itaanzisha mfumo mpya wa pembejeo.
Dkt. Mwanjelwa amesema kuwa ili kuboresha usambazaji wa pembejeo kwa wakulima katika msimu wa mwaka 2017/2018 mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja (Bulk Procurement system- BPS) umeongeza upatikanaji wa mbolea kwa wingi, bei nafuu na wakati.
Aidha, kwa kutumia utaratibu huo bei za mbolea aina ya DAP na UREA zimepungua kwa wastani wa asilimia 30.
“Serikali kupitia mfumo wa ununuzi wa mbolea kwa pamoja hutoa bei elekezi kwa kuzingatia umbali kutoka makao makuu ya wilaya kwenda Kata na vijiji”, alisisitiza Mhe. Dkt. Mwanjelwa.
Akifafanua zaidi, Dkt. Mwanjelwa alisema kuwa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) inaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na pindi ukiukwaji wa bei elekezi unapobainika hatua stahiki zinachukuliwa kwa wahusika.
Serikali katika kuimarisha sekta ya kilimo imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuimarisha kilimo kwa kuwekeza katika pembejeo, mbolea na zana zinazoweza kuikuza sekta ya kilimo ili iweze kuchochea uchumi wa viwanda.

Fahamu mbinu za kuongeza thamani nyama

  Safari ya kuongeza thamani nyama ya mifugo huanzia shambani kwa usimamizi wa ufugaji na uzalishaji. Lishe bora ni muhimu kwa wa ufugaji ...