Friday, April 24, 2026

SUA Yaimarisha Matumizi ya Drones Kufundishia Kilimo cha Kisasa





Rasi wa Ndaki ya Kilimo katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Dkt. Nyambilila Amuri, amesema kuwa chuo hicho kinaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia ya ndege nyuki (drones) katika kufundishia kilimo cha kisasa.


Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Dkt. Amuri alibainisha kuwa matumizi ya drones yanafanyika kwa kushirikiana na kampuni ya Agrimazao. Alieleza kuwa teknolojia hiyo ilianza kutumika tangu mwaka jana, ikiwa na lengo la kuongeza uzalishaji, tija pamoja na ufanisi katika matumizi ya pembejeo za kilimo.


Aidha, alitoa kauli hiyo wakati wa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wanaosomea shahada mbalimbali za Kilimo chuoni hapo, akisisitiza umuhimu wa kuwajengea wanachuo ujuzi wa kisasa unaoendana na mahitaji ya sekta ya kilimo.



Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, Profesa Rafael Chibunda, alisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa chuo kuboresha mitaala yake ili kuandaa wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira.


Aliongeza kuwa chuo tayari kimenunua ndege nyuki tatu na kina mpango wa kuongeza zaidi ili kupanua wigo wa mafunzo kwa vitendo. Pia, chuo kimeboresha matumizi ya teknolojia ya matrekta ili kurahisisha ufundishaji na ujifunzaji wa kilimo cha kisasa pamoja na matengenezo ya mitambo ya kilimo.


Wakizungumzia matumizi ya teknolojia hiyo, baadhi ya wanachuo walieleza kuwa imeongeza ufanisi katika ujifunzaji kwa vitendo na kupunguza changamoto zilizokuwepo katika kilimo cha kizamani.


Elizabeth Salim, mwanafunzi wa Shahada ya Uzalishaji wa Mazao na Usimamizi, alisema kuwa matumizi ya drones yanaifanya sekta ya kilimo kuwa rahisi, rafiki kwa mazingira, na kusaidia kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.


Naye Frank Luhanuza, anayesomea Uchumi wa Kilimo na Kilimo Biashara, alibainisha kuwa teknolojia hiyo inatoa fursa kwa vijana kujiajiri pamoja na kupunguza gharama za uzalishaji, hali inayochochea kuvutia zaidi kizazi cha sasa kujiunga na sekta ya kilimo.


UONGOZI WA MKULIMA JEMBE ...Inatoa pongezi sana kwa chuo cha SUA

No comments:

Post a Comment