(Jovina Bujulu- MAELEZO)
Kuwepo na mfumo wa stakabadhi
ghalani kumekuwa ni mkombozi pekee kwa wakulima wadogo na wa kati kwa
kuwawezesha kupata bei nzuri ya mazao yao, ukilinganisha na bei
zilizokuwa zinatolewa na wafanyabiashara wanaponunua mazao yakiwa
shambani kwa kutumia vipimo ambavyo sio sahihi.
Taarifa iliyotolewa na bodi ya
usimamizi wa Stakabadhi za Ghala imesema kuwa kabla ya mfumo huo
kuanza wakulima walikuwa wakipunjwa bei ya mazao na wafanyabiashara na
kutolea mfano zao la korosho ambapo katika msimu wa 2015/2016, kilo
moja ya korosho ilinunuliwa kwa shilingi 2900 na msimu wa 2016/2017 bei
ilipanda na kufikia shilingi 4,000 kwa kilo ambazo ni sawa na ongezeko
la asilimia 15.9
Mfumo huo umewanufaisha wakulima
kwa kutumia ghala ambazo ziliachwa kwa muda mrefu bila matumizi ambazo
zimekuwa na tija kwa wakulima.
Kupitia ghala hizo zenye ujazo wa
kuanzia tani 200 hadi 5000 na kuendelea wameweza kuhifadhi mazao yao
vizuri na kwa ubora unaotakiwa kwa matumizi ya sasa nay a baadaye.
Aidha, mfumo huo umeongeza ajira
kwa wakina mama na vijana hasa katika maeneo ya kuchambua, kupokea na
kupanga mazao ghalani. Vijana wengi wameajiriwa kwa kazi ya kushusha,
kupanga na kupakia mazao na wameweza kujiajiri katika kilimo baada ya
kuona mfumo huo unavyofanya kazi vizuri na kuwa na uhakika wa soko la
mazao yao.
Wakulima pia wamepata mafanikio
kwa kuwa na uhakika wa vipimo vya mazao yao yanayohifadhiwa ghalani
kupimwa kwa kilogramu na si vinginevyo ambapo kabla ya mfumo huo
wakulima walikuwa wakiibiwa mazao yao kutokana na matumizi ya vipimo
ambavyo si sahihi.
Kwa kuhifadhi mazao yao katika
ghala zenye leseni, wakulima wamekuwa wanatumia mazao hayo kama dhamana
ya kupata mikopo kutoka katika taasisi mbalimbali za fedha. Hii
imewezekana kutokana na wakulima hao kujiunga katika umoja kupitia
vikundi au vyama vya ushirika .
Wafanyabiashara pia wameneemeka
na mfumo huu, ambapo kwa sasa wameweza kupunguza gharama za kufuata
mazao maeneo mbalimbali mazao yanapatikana kwa wingi badala yake mazao
hayo wanayapata katika eneo moja kkwenye ghala zilizosajiliwa na hivyo
kuondoa hatari ya kuibiwa pesa zao na madalali wasio waaminifu.
Mfumo huo pia umekuwa na faida
kwa bodi za mazao katika kuandaa bajeti za mahitaji ya pembejeo na
kuongeza ili kuboresha na kuongeza uzalishaji.
Aidha, mfumo huo umechochea na
kuharakisha uanzishwaji wa soko la bidhaa nchini, kutokana na kuwepo kwa
bidhaa zenye ubora na zinazopatikana kwa wakati. Bodi ya Usimamizi wa
Stakabadhi za Ghala, inatoa wito kwa wakulima kuunga mkono
uhamasishaji wa matumizi ya soko hilo ili kuongeza tija na kasi ya
kukuza biashara ya mazao ya kilimo hapa nchini.
Mfuko wa Stakabadhi Ghalani
ulianza mwaka 2000 ukifadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Bidhaa. Lengo
la mfuko huo ni kuwezesha wakulima kufaidika na ongezeko la bei katika
msimu wa mazao, kuongeza mapato ya wakulima na kuboresha kipato chao
ikiwa ni pamoja na kuwapa wakulima nguvu ya soko kwa kuhamasisha
utumiaji wa vikundi vya wakulima na ushirika.
No comments:
Post a Comment