BATA MZINGA UJASIRIAMALI MPYA KWA WAFUGAJI

BATA MZINGA UJASIRIAMALI MPYA KWA WAFUGAJI
BATA MZINGA UJASIRIAMALI MPYA KWA WAFUGAJI
BATA MZINGA UJASIRIAMALI MPYA KWA WAFUGAJI: Unapotaja ufugaji, wengi wanakimbilia kuku, bata, ng’ombe, mbuzi, kondoo, ni wachache wanaoweza kukutajia  bata mzinga.
Ndege huyu analipa sokoni, ila lazima niseme tangu mapema kuwa ndege hawa wanahitaji matunzo ya hali ya juu. Pia, hula chakula kingi kuliko kuku.
Ukiondoa chakula, bata mzinga wanahitaji kuwa na uhuru wa kula majani kama sehemu ya virutubisho.
Kabla ya kuanza ufugaji wa bata mzinga ni lazima kuhakikisha una chakula cha kutosha, kwa sababu ulishaji wa ndege hawa kadri wanavyokua huwa na gharama kubwa zaidi.
Ni muhimu pia kujifunza kwa undani na kufahamu namna ya kutunza vifaranga wa bata mzinga kwa kuwa hufa kwa urahisi sana.
Pia, unapaswa kujikita kutafuta soko kwa sababu wanapokua ni vigumu kuwatunza kwa muda mrefu kutokana na ukubwa wa gharama ya chakula.
Wafugaji wachache kati ya wengi waliojaribu kuwafuga ndege hawa na kufanikiwa hata kufikia malengo yao ni kutokana na kuzingatia lishe kamili.
Pamoja na hayo, wapo wafugaji ambao walishindwa kutokana na magonjwa pamoja na gharama ya utunzaji.

CHAKULA
Chakula cha bata mzinga hakina tofauti na cha kuku. Vifaranga wanahitaji kupata lishe kamili yenye protini kwa wingi ili waweze kukua vizuri.
Vifaranga kwa siku za awali wanahitaji kiasi cha asilimia 27 ya protini mpaka wanapofikia umri wa wiki sita. Baada ya hapo mfugaji anaweza kupunguza hadi kufikia asilimia 18 na kuendelea  hadi wanapokomaa.
Kutokana na gharama ya kununua chakula kuwa kubwa, unaweza kutumia resheni ifuatayo kwa ajili ya kutengeneza chakula cha bata mzinga wewe mwenyewe.
 Mahindi yasiyokuwa na dawa kilo 5, karanga (5), dagaa (5), mashudu (10) na chokaa (5).

NAMNA YA KUTENGENEZA CHAKULA

Twanga au saga pamoja kiasi cha kulainika kisha walishe vifaranga. Mchanganyiko huu hutegemeana na wingi wa bata mzinga unaowafuga.
Hakikisha kila bata anapata chakula cha kutosha na chenye uwiano ulioelekezwa. Pia, waangalie mara kwa mara kuhakikisha wana chakula cha kutosha.

Hifadhi chakula cha ziada kwenye mifuko au debe kisha weka sehemu isiyo na unyevu.

Bata mzinga huanza kutaga anapofikisha umri wa mwaka mmoja. Ndege hawa wana uwezo wa kutaga kati ya mayai 15 hadi 20 kwa mara ya kwanza kisha kuatamia. Anapoendelea kukua huweza kutaga hadi mayai 30. Hii ni kulingana na lishe nzuri atakayopatiwa.
Bata mzinga anaweza kuatamia mayai 17 hadi 20. Mayai hayo huatamiwa kwa siku 28 na huanza kuanguliwa vifaranga kwa muda wa siku tatu, kuanzia siku ya 28 hadi 31. Baada ya hapo mayai yaliyosalia bila kuanguliwa hutakiwa kutupwa kwa kuwa hayataanguliwa tena na hayafai kwa matumizi mengine.
Baada ya vifaranga kuanguliwa, watenge na mama yao kwa kuwaweka kwenye banda safi lisilopitisha baridi. Unaweza kuwawekea taa ya kandili au ya umeme.
Waziri Mkuu mstaafu akiangalia Bata Mzinga
Waziri Mkuu mstaafu akiangalia Bata Mzinga, Bw, Mizengo Pinda
BANDA
Ni vyema banda liwe limesakafiwa au banda la asili la udongo usiotuamisha maji. Pia, unaweza kutumia banda lenye mbao au mabanzi kwa chini. Unaweza pia kutandaza maranda kwenye mabanda. Hakikisha kuta za banda zimefunikwa vizuri ili kuwakinga dhidi ya baridi.
MAJI
Kama ilivyo ndege wengine, bata mzinga pia wanahitaji kupatiwa maji safi na ya kutosha wakati wote. Wawekee maji katika chombo ambacho hawatamwaga na wanakifikia vizuri.
Hakikisha maji hayamwagiki bandani kwani kwa kufanya hivyo banda litachafuka na kukaribisha magonjwa kwa urahisi. Ni vizuri kuwalisha bata mzinga vyakula vingine kama majani.
Majani husaidia kuwapatia protini: mfano; kunde, fiwi na aina nyingine za majani jamii ya mikunde huhitajika zaidi kwa kiasi cha asilimia  25 hadi 30.

MAGONJWA

BATA MZINGA HUSHAMBULIWA NA MAGONJWA KAMA HOMA YA MATUMBO, MAFUA NA KUHARISHA DAMU. Wanapougua ni rahisi kuambukiza kuku, bata na ndege wengine wanaofugwa kwa haraka sana.
Pia, ndege hawa husumbuliwa na viroboto wanaosababishwa na uchafu wa banda hasa linapokuwa na vumbi.
CHANJO
Bata mzinga wanatakiwa kupatiwa chanjo ya ndui (mara moja kila mwaka), kideri (kila baada ya miezi mitatu), gumboro (kwa muda wa wiki tano, ukiwapa jumatatu, basi unawapatia kila jumatatu ya wiki), na vitamini A mara baada ya kuanguliwa.

Comments

Popular Posts