Katika jitihada za kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na uharibifu wa mazingira, Kikundi cha Nishati Group kilichopo kata ya kahe magharibi Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro, kimeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya rasilimali na uhifadhi wa mazingira.
Hivi karibuni, kikundi hicho kilishiriki katika zoezi la upandaji miti katika Shule ya Sekondari Mangoto, tukio lililolenga kuongeza uoto wa asili, kulinda ardhi dhidi ya mmomonyoko, pamoja na kuwajengea wanafunzi na jamii kwa ujumla uelewa juu ya umuhimu wa miti katika maisha ya kila siku.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mwenyekiti wa kikundi hicho, Rajabu Mvungi, alieleza kuwa lengo kuu la Nishati Group si tu kupanda miti, bali pia kuelimisha wakulima juu ya mbinu bora za kilimo zinazolinda mazingira. Alisisitiza kuwa kilimo kisichozingatia uhifadhi wa mazingira huchangia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo kupungua kwa mvua na kuharibika kwa rutuba ya udongo.
“Tunawahamasisha wakulima kutumia nishati safi badala ya kutegemea kuni na mkaa, ili kupunguza ukataji wa miti. Pia tunatoa elimu ya kuandaa mashamba kwa njia rafiki kwa mazingira, kama vile kilimo mseto, matumizi ya mbolea za asili, na uhifadhi wa maji,” alisema Mvungi.
Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo, kikundi hicho kinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa fedha za kuendesha shughuli zake, ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wakulima na kuendeleza miradi ya nishati safi. Ukosefu wa rasilimali fedha umekuwa kikwazo katika kufikia jamii kubwa zaidi inayohitaji elimu hiyo muhimu.
Wadau wa mazingira na maendeleo wanahimizwa kuunga mkono juhudi za vikundi kama Nishati Group, ambavyo vina mchango mkubwa katika kujenga jamii inayojali mazingira na kutumia rasilimali kwa njia endelevu.
Kwa ujumla, juhudi za Nishati Group zinaonesha wazi kuwa ushirikiano kati ya jamii, shule, na vikundi vya kijamii unaweza kuwa chachu ya mabadiliko chanya katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, huku ikiimarisha sekta ya kilimo kwa njia endelevu na rafiki kwa mazingira.
No comments:
Post a Comment